Social Icons

Monday, April 25, 2011

HARUFU YA DAMU



Urafiki uliochipukia hivi karibuni kati ya mastaa maarufu wa filamu Bongo, Wema Sepetu, Rose Ndauka na Jacqueline Pentezel, umezua mjadala huku wadau wakidai eti una harufu ya damu,

Wakizungumza katika nyakati tofauti, baadhi ya mastaa wanaowafahamu vizuri wasanii hao walioanzisha kampuni yao iitwayo JAROWE walidai kuwa, kutokana na tabia zao kuna uwezekano siku moja wakatibuana.
“Mimi nawafahamu vizuri hawa, wote ni moto wa kuotea mbali na kila mmoja yuko juu, hivi ushawahi kuona mafahari wawili wakakaa zizi moja? Nawaambia ipo siku mtasikia kimenuka, sisi tupo,” alisema mmoja wa wasanii aliyeomba hifadhi ya jina lake.

Mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Jasmine Charles alisema kuwa, yeye alishawahi kuwa na urafiki na wasichana hao kwa nyakati tofauti lakini hawakudumu kutokana na tabia zao.

“Mimi nakwambia wote washawahi kuwa mashoga zangu lakini hatukudumu, sasa leo wameungana, huoni kuna harufu ya damu hapo?” Alihoji mrembo huyo na kuongeza;
“Siwaombei mabaya ila wanatakiwa kuwa makini tu katika kuiendesha kampuni yao kwa nidhamu na kuheshimiana, wamethubutu kufanya jambo la msingi, naamini watafanikiwa.”

Wakizungumzia madai hayo, masistaduu hao ambao tayari wameshaandaa filamu moja walisema kuwa, wanajua mengi yatasemwa lakini wao wako imara na watatimiza kile walicholenga.

“Najua wataongea mengi ila hapa ni kazi tu, sisi wote ni mastaa, tumeamua kuungana ili tutimize ndoto zetu,” alisema Jack.

Naye Wema a.k.a Mrs Diamond alisema: “Wengi hawakutegemea kama sisi tunaweza kufanya kazi pamoja, sasa imekuwa na tunaamini hakuna cha harufu ya damu wala nini, tumedhamiria kuleta mabadiliko.”

0 comments: