INAZUNGUMZWA sana mitaani , dhana hii ya CCM kujivua gamba. Najiuliza, je, huku ni ‘ Kuzaliwa kwa Chama ‘kipya’ au kuzaliwa ‘upya’ kwa chama kikongwe? Unaweza kukiona ninachokiona kadri unavyofuatilia mtiririko wa fikra zangu.
Nionavyo, wengi tumebaki tukijadili kilicho juu ya gamba. Hatuzami kuangalia kilichomo ndani ya gamba. Ndio maana, kama kawaida yetu, tumejikita kwenye kujadili zaidi majina ya watu.
Na tujiulize; ni nini hasa maana ya CCM kujivua gamba? Ni bahati mbaya, kuwa neno kujivua gamba linatoa tafsiri nyingi hasi na chanya. Na wakati mwingine, limewahamisha watu kutoka kwenye hoja za msingi juu ya nini kinachotokea . Mimi nitaelezea kujivua gamba kwa kutoa mfano wa nyumba .
Ndio, CCM ni chama kikongwe. Ni kama nyumba kongwe. CCM wanataka kuikarabati upya nyumba yao. Ipate mwonekano mpya. Kuikarabati upya nyumba kongwe huweza pia kupelekea kuibomoa nyumba yenyewe. Kutakuwa na fito na vipande vya matofali vya kurudishia. Kutahitajika fito na matofali mapya pia. Ndio, fito na matofali mengine yatakuwa ni ya kutupa tu, na ni lazima yatupwe, basi. Na hapo utakuwa umeikarabati upya nyumba yako.
Na nyumba kongwe ya CCM kwa sasa imechakaa, haina mvuto. Wengi hawaipendi, na hususan vijana. Hawa ndio hao walio wengi kwenye kupiga kura. Kwa CCM kurudisha imani ya wapiga kura hawa inahitaji kufanya ukarabati mkubwa wa nyumba yake kongwe. Katika Afrika hii kuna kisa cha Chama tawala kilichochukiwa mno na wapiga kura kiasi kikaamua kubadilisha jina na rangi ya bendera yake ya chama!
Turudi kwenye gamba. Hivyo basi, katika kujivua gamba huku, CCM, kama nyumba kongwe inayofanyiwa ukarabati, yumkini inaweza kubomoka. Hayo yatakuwa ni matokeo ya kawaida kabisa. Ndio, kuna watakaondoka na fito na matofali yao, watakwenda kujenga mahali pengine. Na katika mchakato huu wa kujivua gamba kuna mawili nayaona yatatokea; Mosi, CCM Kuzaliwa Upya au pili, Kuzaliwa kwa Chama kipya. Na mawili hayo yakitokea yatadhihirisha ukweli wa alichoandika Mwalimu Nyerere kwenye kitabu chake; ’ Uongozi Wetu Na Hatima Ya Tanzania’. Hapa kuna mawili, ama kuna Wana- CCM waliosoma kitabu hicho cha Mwalimu bila kukielewa au hawakukisoma kabisa.
Na nini maana ya Kuzaliwa kwa Chama Kipya? Naikumbuka vema Jumamosi ya Februari 5, 1977. Siku hiyo nilibaki na mwezi na wiki moja kabla sijatimiza miaka 11. Ni siku ile Chama Cha Mapinduzi kilipozaliwa. Nikiwa na watoto wanzangu tulikwenda pale ofisi za TANU Ilala Boma kushuhudia tukio lile la kihistoria. Nilichoshuhudia pale Ilala Boma ni ’Kuzaliwa Kwa Chama Kipya’. Niliziona nyuso nyingi za watu wazima zilizojaa matumaini ya siku zijazo, nasi kama watoto, ujio wa Chama kipya ulitujengea matumaini ya baadae.
Na kwa mwanadamu, lililo kubwa ni uwepo wa matumaini.
Na imani ya wananchi kwa viongozi wao ni shina la matumaini yao. Inakuwaje basi mwananchi anapokosa imani kwa kiongozi? Jibu; hukosa matumaini. Atakimbilia popote pale anapoona kuna matumaini. Wahenga walinena; mtoto akikosa titi la mama, atanyonya hata la mbwa. Chama Cha Mapinduzi kihistoria kimekuwa ni kimbilio la wanyonge, lakini sivyo ilivyo kwa sasa.
Na tuamini, kuwa Jakaya Kikwete ameingia katika kazi ya kuongoza Mabadiliko Makubwa ndani Ya CCM. Mwingine atauliza; Je, mabadiliko hayo yatakuwa makubwa kwa kiasi gani? Jibu; ni suala la kusubiri na kuona. Na hapo ndipo tutaweza kutoa hukumu stahili.
Ieleweke, kuwa CCM ni Chama tawala. Kinachotokea ndani ya CCM chaweza kuwa na athari chanya au hasi kwa taifa letu. Na ndio maana, kwa kutanguliza maslahi ya nchi, tuna wajibu wa kumuunga mkono Rais wa nchi na Mwenyekiti wa CCM katika kazi yake hii.
Nimepata kuandika, kuwa ya CCM yanatuhusu sote, wanachama na tusio wanachama. Kwa sasa, CCM inapitia moja ya vipindi vigumu sana tangu kuanzishwa kwake, hivyo basi, nchi yetu nayo inapitia moja ya vipindi vigumu sana tangu tupate uhuru. Hiki ni Kipindi Cha Mpito kuekelea kwenye mabadiliko makubwa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Na hakuna atakayeweza kuyauzuia mabadiliko haya makubwa, maana wakati umebadilika. Chama Cha Mapinduzi kina jukumu la kuyaongoza mabadiliko haya. Na nimepata kuandika, kuwa CCM ina mawili ya kuchagua; kuendanda na mawimbi ya mabadiliko haya, au kukubali kusombwa na kutupiliwa kando.
Yumkini Jakaya Kikwete amezisoma alama za nyakati. Na hakika, sikupata kufikiri, kuwa katika mwaka wa kwanza tu wa awamu yake ya mwisho ya uongozi, Jakaya Kikwete angekifikisha chama chake katika hatua ya kujivua gamba kama tunavyoshuhudia.
Tunaona, CCM imeanza kujivua gamba, lakini hiyo haitoshi. Taifa letu nalo linahitaji kujivua gamba. Na sisi , kama taifa, hatutakuwa wa kwanza, imetokea katika nchi za wenzetu. Kuna mifano hai.
Utawala wa Kikomunisti wa Urusi ya zamani ulianguka mara ile Mikhael Gorbachev alipoanzisha mageuzi makubwa ya kimfumo kisiasa, kiuchumi na kijamii katika Urusi. Mabadiliko haya makubwa ya kimfumo yalipata majina mawili; Perestroika na Glasnot. Perestroika ina maana ya ujenzi mpya na Glasnot ni uwazi .
Kabla ya mageuzi hayo makubwa, Urusi ilikuwa ikikabiliwa na tatizo la kuwepo na fikra za ukale na kukosekana kwa uwazi. Jamii ilijawa hofu, mambo mengi yalikuwa ya kufichaficha. Kulikuwa na usiri mkubwa. Lakini, ndani ya kufichwa huko, kulikuwa na harufu ya uoza mkubwa. Gorbachev, daima atakumbukwa kwa ’ Kuvunja Ukimya’ na kuifanya Urusi kuwa nchi ya kisasa kama inavyoonekana sasa.
CCM ina cha kujifunza kutokana na yaliyotokea Urusi na yanayoendelea sasa katika nchi za Kiarabu na kwingineko. Ni ukweli, kuwa ndani ya CCM na hata Serikalini, kuna watendaji wenye kufanya kazi kama vile tuko kati kati ya miaka ya sabini. Halafu bado ndani ya CCM kuna wanaoshangaa kuona vijana wa leo wakikipa mgongo chama hicho.
Maana , imefika mahali, kuwa moja ya sifa ya kushiriki siasa ndani ya CCM
ni kuwa na uwezo wa ’ kuendekeza fitna na kusema uwongo!’ Na kwa wengine, uongozi ndani ya CCM unapatikana kama vile mtu anayekwenda kununua ng’ombe mnadani.
Na kuna kauli za Wana-CCM zenye kuthibitisha ukweli huu. Mojawapo ilipata kutolewa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama hicho, Phillip Mangula aliyepata kutamka; ” Isifike mahala CCM ikatangaza tenda za uongozi!”.
Naam. CCM wanajivua gamba. Kila la kheir Chama Cha Mapinduzi.
0 comments:
Post a Comment