Mwakilishi wa Kampuni ya Fleva Unit ambayo ndiyo imekabidhiwa studio ya kurekodia muziki (Mastering Studio) na Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete, Said Fella (kushoto) akitoa ufafanuzi juu ya vifaa hivyo Jumatatu wiki hii kwenye Jukwaa la Sanaa BASATA. Katikati ni Katibu Mtendaji wa BASATA, Ghonche Materego na Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia Sanaa Bi. Angela Ngowi.
Na Mwandishi Wetu
Serikali kupitia Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo imesema kwamba studio ya kurekodia muziki (mastering studio) iliyotolewa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete ni ya wasanii waliyoiomba na hao ndiyo waliokabidhiwa.
Msimamo huu wa serikali umekuja kufuatia kuwepo kwa mkanganyiko miongoni mwa wadau wa sanaa hususan muziki wa kizazi kipya juu ya nani hasa amekabidhiwa studio hiyo na umetolewa na Mkurugenzi Msaidizi Sanaa, Bi.Ngowi wiki hii kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).
Alisema kwamba, studio hiyo ya Rais Kikwete imetolewa kufuatia maombi zaidi ya kumi na moja yaliyotolewa na wasanii waliohudhuria sherehe za miaka mitatu toka kuanzishwa nyumba ya vipaji nchini (THT) na imekabidhiwa kwa wasanii hao waliokuwepo kupitia Kampuni ya Fleva Unit ambayo imesajiliwa kwa msajili wa makampuni nchini (Brela).
“Msimamo wa Rais Kikwete ndiyo huu, studio ameitoa kwa wasanii waliomuomba na wengine wanaotaka kusaidiwa wapeleke maombi yao milango haijafungwa” alisisitiza Bi. Ngowi.
Aliongeza “Najua kauli hii itawaumiza wengi wenu hapa ila lazima mjue kwamba, serikali haifanyi kazi kupitia maneno matupu, wizara kwa muda mrefu imekuwa kimya ikifuatilia msimamo wa Rais mwenyewe kuhusu studio hii na tayari tumeshapata kauli yake katika maandishi ndiyo hiyo niliyowaambia”.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa BASATA aliwaomba wadau wa sanaa hasa chama kilichosajiliwa kisheria cha wasanii wa muziki wa kizazi kipya cha Tanzania Urban Music Association (TUMA) kutumia fursa hiyo kuomba msaada kwa Rais huku akisisitiza kwamba, Baraza lake litapitisha maombi hayo.
“Ndugu zangu kauli ya Rais ni ya mwisho. Kumekuwa na maneno mengi sana juu ya hili nadhani leo tumepata majibu kutoka sehemu husika na malumbano yatakuwa yameisha” Aliongea Materego huku akisisitiza kwamba TUMA ndicho chama cha wasanii wa kizazi kipya kinachotambulika na BASATA haitakuja kusajili Chama kingine.
Awali Mbunge wa Mbeya Mjini ambaye pia ni moja ya waasisi wa chama hicho, Joseph Mbilinyi (Sugu) sambamba na wadau wengi wa Jukwaa la Sanaa walihoji masuala mbalimbali kuhusu studio hiyo huku wakihoji uhalali wa vifaa hivyo kukabidhiwa watu binafsi badala ya Wizara, BASATA au TUMA ambavyo ni vyombo vinavyotambulika kisheria serikalini.
Walihoji pia wapi vifaa hivyo vya studio vilikuwa kwa muda wote wa miaka mitatu toka vitolewe kwani kwa mujibu wa kauli ya Mwakilishi wa Kampuni ya Fleva Unit, Said Fella kwenye Jukwaa hilo la Sanaa, Kampuni hiyo imepata usajili wiki moja iliyopita.
Mjadala huo kuhusu Studio ya Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete ulitanguliwa na Mada ya Dhana na Mtizamo Juu ya Ukuzaji wa Fani ya Usanifu Majengo kama Tanzu ya Sanaa Kutokana na Urithi wa Utamaduni Wetu iliyowasilishwa na Dkt. Lwamayanga kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU).
Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Kulia) akihoji masuala mbalimbali kwenye Jukwaa la Sanaa BASATA wiki hii kuhusu Studio iliyotolewa kwa wasanii na Rais Jakaya Kikwete miaka mitatu iliyopita. Kulia kwake ni Mratibu wa Jukwaa hilo, Ruyembe C.Mulimba.
Mkurugenzi wa Idara ya Utamaduni kitengo cha Sanaa kutoka Wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo, Bi. Ngowi akitoa tamko la Rais Jakaya Kikwete kuhusu Studio aliyoitoa kwa wasanii kwenye Jukwaa la Sanaa. Katikati ni Katibu Mtendaji wa BASATA, Bw. Materego na Said Fella.
Katibu Mtendaji wa BASATA, Bw. Materego akisisitiza jambo kwenye Jukwaa hilo kuhusu Studio ya kurekodia Muziki (Mastering Studio) iliyotolewa kwa wasanii na Rais Jakaya Kikwete.
Msanii wa Hip Hop, Rado naye alikuwa sehemu ya wasanii kibao waliofika kutaka kupata maelezo kuhusu Studio hiyo ya JK kwa wasanii.
Dtk. Lwamayanga kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi (RAU) akiwasilisha Mada yake kuhusu Dhana na Mtizamo Juu ya Ukuzaji wa Fani ya Usanifu Majengo kama Tanzu ya Sanaa Kutokana na Urithi wa Utamaduni Wetu kwenye Jukwaa la Sanaa BASATA wiki hii. Kushoto kwake ni Bw. Materego Katibu Mtendaji wa BASATA.
Sehemu ya wadau wa Sanaa waliohudhuria kwenye Jukwaa la Sanaa wakifuatilia kwa makini masuala mbalimbali yaliyokuwa yakijitokeza.
0 comments:
Post a Comment