KUSIKITISHWA NA TUKIO LA MILIPUKO YA MABOMU LILILOTOKEA GONGO LA MBOTO JIJINI DAR ES SALAAM TAREHE 16 FEBRUARI, 2011
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) inaungana na Watanzania wote nchini kuomboleza maafa yaliyotokea kufuatia milipuko ya mabomu katika ghala la kuhifadhia silaha katika kambi ya Jeshi la wananchi (JWTZ) iliyopo Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam.
Tume imesikitishwa na tukio hilo ambalo kutokea kwake kumesababisha uvunjifu wa haki za msingi za binadamu ambazo ni haki ya kuishi na haki ya kumiliki mali.
Ni wazi kuwa milipuko hiyo imegharimu maisha ya watu ambapo mpaka sasa inakadiriwa watu wapatao 23 wameripotiwa kufa na kuacha mamia ya watu wakiwa wamejeruhiwa vibaya, baadhi yao wakibaki bila makazi.
Aidha, Tume inampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na wadau wote yakiwemo mashirika na wananchi kwa hatua za haraka walizozichukua kuwahami waathirika wa milipuko hiyo kwa kuwapatia misaada na huduma zinazostahili.
Wakati huo huo, Tume inatoa wito kwa Kamati ya Ulinzi na Usalama iliyoundwa na Rais kuzingatia misingi ya Utawala Bora wakati wa kutoa huduma na fidia kwa waathirika, kwani kumekuwa na tabia kunapotokea matukio kama haya watu wasio waadilifu hutumia nafasi hii kwa mamlaka waliyopewa kutotenda haki kwa waathirika na badala yake hujinufaisha wao wenyewe na wale wanaostahili kupata haki wanabaki mikono mitupu.
Tunawapa pole wale wote walioathirika na milipuko hii na tunawaomba wawe wavumilivu katika kipindi hiki kigumu wakati serikali ikiandaa taratibu za fidia.
Jaji Kiongozi (Mstaafu) Amiri Ramadhani Manento
MWENYEKITI
21. 02. 2011
0 comments:
Post a Comment