Social Icons

Friday, February 4, 2011

MANJI AMPONDA MENGI


Mkurugenzi wa Kampuni ya Quality Group, Yusuph Manji (kulia) akiongozana na Katibu wake, Mhingo Rweyemamu, wakati wakiingia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam Jana mchana kwa ajili ya kuwasilisha vielelezo na kutoa ushahidi katika kesi yake dhidi ya Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Regnald Mengi. Katika kesi hiyo Manji alimtaka Mengi kumlipa fidia ya Sh 1 tu pamoja na kumuomba radhi kupitia Televisheni yake ya ITV kwa muda wa siku saba mfululizo.


Yusuph Manji, akizungumza na wakili wake Mabele Marando, wakati alipoingia kwenye Chumba cha mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam jana, kwa ajili ya kutoa ushahidi na kuwasilisha vielelezo vya kesi yake dhidi ya Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Regnald Mengi.


Manji akipitia faili lake kabla ya kuingia katika chumba cha Mahakama kuanza kutoa ushahidi.

MFANYABIASHARA maarufu jijini Dar es Salaam, Yusuf Manji, ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kuwa tuhuma zote dhidi yake zilizotolewa na Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP Ltd, Reginald Mengi, za kuwa ni fisadi papa, ni uzushi mtupu na zimemshushia hadhi yake.

Akitoa ushahidi leo mbele ya Mahakama hiyo, Manji alisema kutokana na kauli aliyoitoa Mengi kupitia vyombo vya habari, imesababisha aonekane mtu asiyefaa katika jamii, na familia yake inataka kumtenga.

“Tuhuma zilizowekwa na Mengi zimeshusha heshima yangu katika jamii, wafanyakazi wangu, familia za wafanyakazi wangu, wabunge hata familia yangu na familia inataka kuondoka,” amedai Manji.

Manji ametoa madai hayo katika kesi hiyo ambayo anadai fidia ya Sh moja kwa madai ya kudhalilishwa na Mengi katika kipindi kilichorushwa kupitia vituo vyake vya televisheni na kwenye magazeti.

Akielezea hadhi aliyonayo mbele ya jamii, Manji alidai kuwa klabu ya soka ya Yanga imemteua kuwa mfadhili, na pia alionesha baadhi ya barua ambazo zilikuwa zikimpa mialiko katika shughuli mbalimbali za kijamii ikiwamo ya mahafali ya kumaliza kidato cha sita kwa wanafunzi wa Shule ya Benjamin Mkapa, jijini.

Kesi hiyo iko mbele ya Hakimu Aloyce Katemana, na Manji anawakilishwa na mawakili Mabere Marando, Beatus Malima, Dk. Ringo Tenga na Richard Rweyongeza.

Manji aliwasilisha mahakamani CD ya video iliyokuwa ikionesha Mengi akiongea kupitia televisheni na akimtaja Manji kuwa ni fisadi papa na kwamba anawanyonya watu wa hali ya chini.

Manji alidai tuhuma hizo si za kweli, bali anajishughulisha na kuwasaidia watu.

Aidha, alikanusha kumiliki nyumba Amerika na Afrika Kusini, akidai hana nyumba yoyote aliyoinunua yeye, bali nyumba zote ni za baba yake ambaye alifariki na kumuachia mama yake ambaye kuna nyumba ambazo alimpatia kama zawadi, na kwamba hata nyumba anayoishi ni ya baba yake.

Alidai Mengi pia amemtuhumu kumtishia maisha yake kuwa atamuua jambo ambalo hajawahi kulifanya, “Hii sio mara ya kwanza Mengi kunituhumu kumtishia maisha yake mara kadhaa amefanya hivyo,” amedai Manji.

Wakati huo huo, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemtaka Mhasibu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Lilian Chengula anayetuhumiwa kuiba fedha za shirika hilo Sh bilioni 1.3, kuwasilisha ombi la dhamana Mahakama Kuu kwa sababu Mahakama hiyo haina kibali cha kusikiliza shauri la uhujumu uchumi.

CHANZO: HABARILEO

0 comments: