Makamu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Benno Malisa.
Katika hali inayofananishwa na uasi, Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), umewarushia makombora wasaidizi wa Rais Jakaya Kikwete wakiwemo baadhi ya mawaziri kuwa hawamsaidii kutatua kero za wananchi hivyo kusababisha malalamiko yasiyo kwisha.
Pia umeitaka serikali isitishe uamuzi wake wa kutaka kuilipa fidia kampuni ya Dowans Tanzania Limited Sh. bilioni 94 kama fidia ya kusitisha mkataba kati yake na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
UVCCM imesema badala yake suala hilo lipelekwe bungeni kujadiliwa upya ili kuwajua walioiingiza serikali kwenye hasara hiyo kisha wawajibike kulipa deni hilo.
“Nchi hii ina matatizo mengi sana, wananchi wanaishi maisha ya shida hivyo haiwezekani kuilipa kampuni hewa kiasi kikubwa kama hicho cha fedha, waliohusika na hasara hiyo watafutwe na washurutishwe kulipa,” alisema Katibu Mkuu wa UVCCM, Martine Shigela, akisoma maamizimio yaliofikiwa na Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la umoja huo mbele ya wahariri na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.
UVCCM iliomba kukutana na Jukwaa la Wahariri ili kuelezea msimamo wao kuhusu mambo mbalimbali ya kitaifa.
Shigela alisema haiingii akilini mmiliki wa Dowans ajulikane na alipwe fidia ya Sh. bilioni 94 wakati kampuni iliyommilikisha mkataba Richmond asijulikane mmiliki wake.
Shigela alisema Dowans walitajwa na serikali kuwa ndio walionunua mali za Richmond, hivyo wanawajibika kuisaidia serikali kuwataja wamiliki halali wa Richmond ili wawajibike kulipa fedha hizo badala ya serikali.
“UVCCM tunataka hoja hii irudi tena bungeni ili Watanzania tujue nani kaifikisha serikali yetu hapa ilipo. Kama ni Tume ya Dk. Harrison Mwakyembe ieleze kama ilishiriki kulidanganya Bunge na iwajibike na kama ni serikali, basi imtake huyo Richmond ambaye ndiye aliyehamishia mali zake kwa Dowans atakiwe kulipa badala ya fedha za walipa kodi wa Tanzania ambazo zingesaidia shughuli za maendeleo,” alisema.
Kuhusu Bodi ya Mikopo kwa Vyuo vya Elimu ya Juu (HESLB), Shigela alisema Rais Jakaya Kikwete anapaswa kuivunja kwani imekuwa ikifanya kazi kama kinyonga na kusababisha matatizo na migomo isiyo na kikomo kwa wanafunzi.
Alisema UVCCM hauko tayari kuona vijana wenzao wakiteseka kwa ubinafsi na ukiritimba uonaosababishwa na watendaji wachache wa HESLB.
“UVCCM imebaini kuwa kuna urasimu unaofanywa na watendaji, mfano mmoja haiingii akilini Chuo Kikuu Mkwawa wagome leo wakidai posho halafu kesho yake wapate posho zao baada ya mgomo, hapo inaonekana dhahiri kuna uzembe tu…Hali hii haikubaliki popote pale duniani hivyo serikali iwawajibishe wahusika mara moja ili tabia kama hiyo isijirudie,” alisema.
Akizungumzia mawaziri wanaolumbana kwenye vyombo vya habari, Shigela alisema UVCCM inalaani kitendo hicho na iliwataka mawaziri wanaofanya hivyo kuacha mara moja na kama wamechoka waachie ngazi na kuwapisha vijana wengine wenye nia njema ya kuongoza kwa kufuata maadili ya taifa.
Alisema inasikitisha kuona hata wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho (NEC) na wale wa Kamati Kuu (CC) wakilumbana kila kukicha kwenye vyombo vya habari.
Akizungumzia hali ya siasa nchini, Kaimu Mwenyekiti wa umoja huo, Beno Malisa, aliishauri serikali ichukue maamuzi magumu ili kukinusuru chama na serikali yenyewe.
Alisema wajumbe wa NEC na CC waache kutoa kauli tata ambazo zinasababisha chuki na uhasama ndani ya chama hicho.
“Leo utasikia mjumbe wa NEC kasema hivi kesho yake unasikia mjumbe wa CC kasema vile, hii hali hatutaivumilia kabisa na kama kuna kiongozi anayejiona ni bora kuliko wanachama wengine anajidanganya na iko siku tutamtaja hadharani,” alisema.
“Viongozi hao watambue kuwa wao walipokuwa vijana hawakurithishwa chuki na uhasama, vivyo hivyo na sisi hatutaki turithishwe uhasama na tunawaomba waache mara moja kabla hatujawataja kwa majina,” alisema.
Alisema limekuwa jambo la kawaida mawaziri kulumbana waziwazi kuhusu masuala yanayohusu uamuzi wa serikali, ingawa waliapa kulinda siri za serikali.
“Haiwezekani leo Waziri anasema hivi kesho yake Naibu Waziri anasema vingine, kama kuna jambo wanapaswa kukaa pamoja na kutoa msimamo unaofanana ... Hii hali hatuipendi na hatutaki iendelee kabisa inatutia aibu,” alisema.
Alisema iwapo ushauri walioutoa hautafanyiwa kazi, watapanga maandamano ya vijana nchi nzima na kutaja hadharani majina ya viongozi wa CCM na mawaziri ambao wanachafua hali ya hewa ndani ya chama na serikalini.
Naye Mbunge wa Viti Maalum, Zainabu Kawawa, ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya umoja huo, alisema serikali imeshindwa kutatua kero za vijana na matokeo yake wengi wamekuwa wakijihusisha na vitendo viovu.
Alisema maelfu ya vijana wanamaliza masomo kila mwaka, lakini serikali imeshindwa kuwatafutia fursa za ajira kutokana na uzembe wa baadhi ya viongozi.
“Ukosefu wa ajira kwa vijana ni uzembe tu wa baadhi ya viongozi wanaofanya kazi kwa mazoea tu, mfano ni huu mgomo wa juzi, wanafunzi wanagoma leo kesho yake wanapewa posho…Hii inatoa taswira kwamba kuna watu wameamua kwa makusudi kuwa wazembe,” alisema na kuongeza:
“Ndiyo sababu tunaomba serikali ivunjilie mbali bodi ya mikopo maana hawawalipi wanafunzi hadi wagome, tunataka serikali ya CCM iwawajibishe hawa viongozi wa bodi haraka maana wameshindwa kazi.”
Alisema vijana wengi wamekuwa wakijihusisha na maandamano kila yanaopotokea, lakini wangekuwa na kazi za kufanya wasingefanya hivyo.
Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha, James Millya, alisema Watanzania bado hawajaambiwa ukweli kuhusu ni nani mmiliki wa kampuni ya Richmond.
Alisema kuna umuhimu serikali ikaacha kumung’unya maneno na ikawataja wamiliki wake kwani lazima itakuwa inawafahamu.
“Watajwe na wawajibike kulipa deni la Sh. bilioni 94 maana wao ndio waliosababisha na serikali isitoe hata senti yake maana hizo ni fedha nyingi sana na Watanzania wanashida nyingi zinazohitaji kutatuliwa kwa fedha,” alisema.
Mjumbe kutoka Zanzibar, Raha Ahmada Ali, alisema wanafunzi wa Zanzibar wanasumbuka sana kupata mikopo, hivyo wameshauri serikali iivunje bodi hiyo na kuweka viongozi wapya.
“Hii bodi haina manufaa kwetu kabisa maana wanafunzi kule wanadhalilika vya kutosha na kwa kweli hatuoni sababu gani bodi hiyo iendelee kuwepo,” alisisitiza.
Hii ni mara ya kwanza UVCCM kujitokeza hadharani kuingia katika malumbano na serikali moja kwa moja, lakini pia kutoa msimamo ambao unaacha maswali mengi hasa juu ya Dowans.
Ingawa umma umechachamaa juu ya Dowans, suala la kuirudisha bungeni inaweza kuwa ngumu hasa ikizingatiwa kwamba suala hilo kwa sasa lipo mahakamani kwa maana ya kukamilika kwa mtiririko wa kisheria wa hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC) dhidi ya Tanesco katika kesi iliyofunguliwa na Dowans.
Wajumbe waliohudhuria kiko cha jana ambacho duru zinasema kiliendelea hadi usiku wa manane ni pamoja na Malisa, Shigela, Naibu Katibu Mkuu, Athmani Kizito na Mkuu wa Idara ya Utawala Makao Makuu, Martin Mulele.
Wengine ni Mkuu wa Idara ya Uhamasishaji, Ester Bulaya; Ridhiwani Kikwete; Mathayo Marwa; James Millya; Kawawa; Suleiman Musin na Hamisi Omar.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment