Social Icons

Friday, September 16, 2011

WAKUU WA MIKOA KUAPISHWA LEO IKULU,

KIKWETE AVUNJA UKIMYA, ATEUA WAKUU WA MIKOA WAPYA 15 AWAKUMBUKA MAWAZIRI WA ZAMANI

Na Musa Mateja

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dk. Jakaya Khalfan Mrisho Kikwete, ameondoa dukuduku kwa wananchi waliokuwa na hamu kubwa juu ya uteuzi wa Wakuu wa Mikoa, baada ya zoezi hilo kufanyika juzi Septemba 14 mwaka huu ambapo aliwateua Wakuu wa Mikoa 15 wapya, miongoni mwao wakiwa ni Manaibu waziri wa zamani na kuwapandisha vyeo wakuu wa wilaya 11 huku wengine saba wakielezwa kwamba wamestaafu kwa mujibu wa taratibu.

Rais Kiwete amewateua waliokuwa Manaibu Waziri watatu ambao ni Mwantumu Mahiza, Ludovick Mwananzila na Joel Nkaya Bendera.

Taarifa ya Ofisi ya Waziri Mkuu iliyotolewa Dar es Salaam juzi iliwataja wakuu wa wilaya waliopandishwa vyeo na mikoa yao katika mabano kuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, John Tupa (Mara), DC wa Morogoro, Said Mwambungu (Ruvuma), Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Chiku Gallawa (Tanga), DC wa Ilala, Leonidas Gama (Kilimanjaro), DC wa Newala, Dk. Rehema Nchimbi
(Dodoma), Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Elaston Mbwillo (Manyara).

Wengine ni DC wa Karagwe, Kanali Fabian Massawe (Kagera), DC wa Mvomero, Fatma Mwassa (Tabora), DC wa Manyoni, Ali Rufunga (Lindi), DC wa Kilombero, Mhandisi Ernest Ndikillo (Mwanza), DC wa Bagamoyo, Magesa Mulongo (Arusha).

Aidha, mbunge wa viti maalum (CCM) , Mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Stella Manyanya ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.

Katika uteuzi huo, Mahiza anakwenda Mkoa wa Pwani, Bendera ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro huku Mwananzila akitupwa mkoa wa Shinyanga.

Kabla ya uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Mahiza alikuwa ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi pamoja na Mwananzila ambapo Bendera alikuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo.

Waliobadilishwa vituo vya kazi ni Abbas Kandoro anayekwenda Mbeya akitokea Mwanza, Said Mecky Sadik anayehamia Dar es Salaam akitokea Lindi, Christine Ishengoma anayekwenda Iringa akitokea Ruvuma, Luten Kanali Issa Machibya kutoka Morogoro kwenda Kigoma na Kanali Joseph Simbakalia anakwenda Mtwara akitokea Kigoma.

Wakuu wa Mikoa waliostaafu ni Mohamed Babu aliyekuwa Kagera; Isidore Shirima (Arusha), Kanali Anatory Tarimo (Mtwara), John Mwakipesile (Mbeya), Kanali Enos Mfuru (Mara), Brigedia Jenerali Dk Johanes Balele (Shinyanga) na Meja Jenerali Said Kalembo (Tanga).

Wengine wanne waliostaafu ambao watapangiwa vituo vingine vya kazi ni Amina Mrisho aliyekuwa Pwani, Dk James Msekela aliyekuwa Dodoma, Abeid Mwinyimusa aliyekuwa Tabora na Daniel Ole Njoolay wa Rukwa.

Taarifa hiyo ya Ofisi ya Waziri Mkuu inasema:

Wakuu wa mikoa mipya minne ya Simiyu, Geita, Katavi na Njombe itakayoundwa baada ya taratibu kukamilika watatangazwa baadaye.

Wakuu wa mikoa hao wanatarajiwa kuapishwa leo majira ya saa kumi jioni katika Viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam.

0 comments: