Aliyekuwa mbunge wa Igunga, Rostam Aziz.
MBUNGE wa Igunga, Rostam Aziz (CCM), ametangaza rasmi kujivua nyadhifa mbili ndani ya chama chake hicho ambazo ni ubunge na ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (M-nec).
Rostam alitangaza uamuzi huo jana katika Ukumbi wa Sakao, uliopo mjini Igunga alipokuwa akuzungumza na wazee wa CCM wa jimbo la Igunga, mkoani Tabora.Katika hotuba yake iliyochukua takriban dakika 40, kuanzia saa 8:41 mchana hadi saa 9:20 jioni, Rostam alisema kuanzia sasa yeye ni mwanachama wa kawaida wa CCM.
Rostam alisema uamuzi wake huo, pamoja na mambo mengine umetokana na wanasiasa uchwara wanaoendesha siasa za kupakana matope baada ya Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Rais Jakaya Kikwete, kutangaza mpango wa kujivua gamba.
"Nimepata msukumo wa kuamua kuachia nafasi zangu zote za uongozi ndani ya chama, nikianzia na ile ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa nikiuwakilisha Mkoa wa Tabora na hii ya ubunge wa Igunga ambazo kama si kwa baraka za chama changu, nisingelikuwa nazo," alisema Rostam.
Aliendelea kusema: "Napenda kuliweka hili sawa sawa. Uamuzi wangu wa kuachia nafasi zangu zote za uongozi nilizopata kwa tiketi ya CCM haukutokana na wala haumaanishi kukubaliana na shinikizo lililopotoshwa kuhusu azma ya utekelezaji wa dhana ya kujivua gamba, la hasha, bali dhamira ya dhati ya kuachana na siasa hizi uchwara (gutter politics) na kutumia muda wangu kushughulika na biashara zangu."
Rostam alisema amefikia uamuzi huo ili kujenga heshima na imani machoni pa wanachama na wananchi wengine na viongozi ambao baada ya kujitoa, anaamini watapata fursa ya kutafakari upya changamoto nyingine mbadala zinazowakabili.
Hata hivyo, alitahadharisha kwamba, kutokana na mazingira yalivyo, anaamini kuna watu watatumia uamuazi wake huo kuipotosha jamii kuhusu hatima yake kisiasa."…..natambua vyema kwamba, watatokea watu ndani ya chama chetu na nje ambao watafanya kila juhudi kupotosha, au kupindisha ukweli kuhusu hatima yangu ya kisiasa baada ya kujiweka kando na kujipa mimi mwenyewe na chama changu fursa ya kutafakari kwa kina majaliwa yangu na ya nchi yangu katika siku zijazo," alisema na kuongeza:
"Nafanya hivyo nikiwa na imani thabiti kwamba, uamuzi wangu huu, hususani ule wa kuachia nafasi yangu ya ubunge, utakipa fursa nyingine CCM ya kuendelea kuliongoza jimbo letu la Igunga katika kipindi cha miaka minne ijayo kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015."
Kwa mujibu wa Rostam, uamuzi wake wa kubakia kuwa mwanachama wa kawaida na mtiifu wa CCM, utakuwa chachu kwa chama hicho na Serikali yake kuwatumikia wananchi kwa Ari Zaidi, Kasi Zaidi na Nguvu Zaidi."Wosia wangu kwa wanasiasa wenzangu, waandishi wa habari na Watanzania wenzangu kwa ujumla, ni kuwa tunahitaji kuisaidia nchi yetu kwa kufanya siasa zenye mwelekeo wa kujenga ambazo ndiyo hasa zinapaswa kuwa siasa kwa maana halisi ya neno hilo," alisema.
Kujivua gamba
Kabla ya kutangaza kujiuzulu nyadhifa hizo, Rostam alichukua muda mwingi kueleza dhana nzima yakujivua gamba, akisema kuwa baadhi ya viongozi wapya wa chama hicho wameipotosha.Alisema dhamira ya kufanya mabadiliko ya ndani ya CCM iliyotangazwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Kikwete, wakati wa kilele cha maadhimisho ya miaka 34 ya kuzaliwa kwa CCM mjini Dodoma ilitekelezwa vizuri, lakini akadai kwamba ilipotoshwa na wajumbe wawili wa Sektretarieti mpya ya chama hicho.
Rostam alisema, Rais Kikwete aliyafananisha mabadiliko hayo na tabia ya kawaida na ya asili ya nyoka ‘Kujivua Gamba’ na kwamba, hatua ya kwanza ya utekelezaji ilifanyika mjini Dodoma wakati vikao vikuu vya CCM ambavyo yeye alikuwa mjumbe wake.
Alisema wakati wa kikao hicho, wajumbe wote wa Kamati Kuu na wale wa Sekretarieti ya CCM wakati huo kwa kauli moja, walikubaliana kujiuzulu, lengo likiwa ni kumpa Mwenyekiti wao (Rais Kikwete) fursa ya kufanya mabadiliko ya uongozi yatakayotoa nafasi ya kupata mwelekeo mpya wa Chama.
"... Chama kilipata safu mpya ya uongozi iliyotokana na kuundwa kwa Sekretarieti inayoongozwa na Katibu Mkuu wetu mpya, Mhe. Wilson Mukama na Kamati Kuu iliyokuwa na sura tofauti na ile ya awali," Rostam alisena na kuendelea:
"Wakati tukitafakari na kuangalia mustakabali mpya wa kisiasa ndani ya chama chetu, ghafla yalianza kutokea mambo ambayo chokochoko zake zilianza kusikika tangu tukiwa ndani ya Kamati Kuu, ambayo ilijiuzulu baadaye."
Awatuhumu Nape, Chiligati
Kwa mujibu wa Rostam, baada ya kumalizika kikao cha Nec ambacho kilichagua wajumbe wapya wa Kamati Kuu na kuidhinisha uundwaji wa Sekretarieti mpya, dhana ya kujivua gamba ilianza kuchukua tafsiri na mwelekeo tofauti.Kada huyo wa CCM aliwatuhumu Naibu Katibu Mkuu (Tanzania Bara), John Chiligati na Katibu wa Idara ya Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, kwa kile alichodai kwamba walipotosha uamuzi wa NEC.
“….walisikika wakitangaza kwamba Halmashauri Kuu ya Taifa ilikuwa imefikia uamuzi wa kuwapa siku tisini walioitwa watuhumiwa wanaokabiliwa na tuhuma za ufisadi ndani ya chama kujitoa katika nafasi zao za uongozi, vinginevyo watafukuzwa na chama," alisema.
"Baada ya kushinikizwa sana na vyombo vya habari wawataje kwa majina wanasiasa waliokuwa wakituhumiwa kwa ufisadi ambao ni wajumbe wa NEC ambao wanapaswa kujiuzulu nyadhifa zao, wajumbe hao wa Sekretarieti walikwenda mbele zaidi," alisema.
Alisema awali waliwaeleza waandishi wa habari kwamba, majina ya watuhumiwa yalikuwa yakifahamika kutokana na kuhusishwa katika kashfa tofauti kama zile za Richmond, EPA na ununuzi wa rada na kwamba, baadaye viongozi hao walikaririwa wakitaja majina ya wanasiasa watatu kuwa ndiyo waliolengwa na uamuzi huo wa NEC.
"Nilishangazwa na kushitushwa na porojo na fitina za kisiasa zilivyofinyangwa kwa mara nyingine baada ya kusikia jina la mbunge wenu ambaye ni mimi, likitajwa kuwa miongoni mwa yale matatu ya viongozi waliokuwa wakitakiwa, eti kupima wenyewe na kisha kuchukua uamuzi wa kujiuzulu nafasi zao za uongozi ndani ya NEC katika kipindi cha siku tisini," alisema na kuongeza:
“Mshangao na mshituko wangu haukusababishwa na kutajwa jina langu, la hasha, bali namna uamuzi halisi wa NEC na hususani dhana nzima ya ‘kujivua gamba’ ilivyoweza kupindishwa na wajanja wachache na kisha kuendeshwa kwa maslahi binafsi ya kikundi fulani cha watu."
Alisema pia alishtushwa na hatua ya viongozi wa CCM kukivisha kikao cha NEC uamuzi ambao msingi wa hoja zake ni vita vya makundi ya kisiasa yaliyo ndani ya CCM kwa upande mmoja na propaganda za vyama vya siasa vya upinzani na vyombo vya habari kwa upande mwingine.
“Tatu, nilishangazwa na kushitushwa na ujasiri ambao umekuwa ukioneshwa na baadhi ya viongozi wetu wapya wa Sekretarieti wanaolitaja jina langu na kulihusisha na kile wanachokiita ufisadi ambao hata ukweli wa kimazingira na kihistoria, ukiachilia mbali ushahidi wa wazi umeshathibitisha kwamba, ni porojo za kisiasa zilizotokana na makovu na matarajio ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 na ule ujao wa 2015,” alisema Rostam.
Alisema mbali ya kwamba amewahi kueleza kupitia vyombo vya habari kwamba hajapata kujihusisha na vitendo vya ukiukwaji wa maadili ya uongozi au rushwa, hakuna ushahidi wowote uliotolewa unaomuhusisha na kashfa yoyote miongoni mwa zile zilizotajwa.
Jimboni Igunga
Akiziungumzia utendaji wake ndani iya jimbo hilo, Rostam alisema "katika kipindi hicho chote cha utumishi wangu, nyinyi wazee wangu mmekuwa mhimili muhimu ambao umeniwezesha kutimiza wajibu wangu kwa bidii kubwa, maarifa na nidhamu ya hali ya juu nikitambua namna ambavyo mmekuwa na imani kubwa juu yangu".
Alisema miongoni mwa mafanikio yaliyofikiwa ni kuwepo kwa umeme na taa barabarani, mfuko wa afya ya jamii kwa kila kaya, zahanati kila kijiji na shule nyingi kuliko idadi ya kata zilizomo kwenye wilaya.
"Nayasema haya nikitambua kwamba, kama ilivyo katika maeneo mbalimbali hapa nchini, mafanikio makubwa tuliyoyapata katika nyanja za elimu, afya, makazi bora na kilimo katika kipindi chote ambacho mmendelea kuniamini kuwa mbunge wenu, kwa miaka 18 sasa.
"
Kauli ya Nape
Jana Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Nape hakutaka kuzungumzia suala hilo, hata baada ya gazeti hili kumtafuta afanye hivyo.Katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, aligoma kuzungumzia suala hilo, badala ya alisisitiza waandishi kutumia habari aliyowaambia.
Baadaye jioni alipotafutwa kwa simu yake ya mkononi, alijibu kwa kifupi," Niko kikaoni, nitumie ujumbe". Hata hivyo, baada ya kutumiwa ujumbe hakujibu chochote na simu yake ikawa imefungwa muda wote.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, John Chiligati, hakupatika kuzungumzia suala hilo baada ya simu yake ya mkononi kuita muda mwingi bila kupokelewa.
Miaka 18 ya Ubunge wa Rostam
Ramadhan Semtawa
ROSTAM Abdulrasul Aziz, ni msomi mwenye shahada ya uchumi, mwanasiasa na mfanyabiashara maarufu nchini.
Aliingia katika siasa kwa mara ya kwanza mwaka 1994 alipogombea ubunge jimbo la Igunga katika uchaguzi mdogo ulioitishwa kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Charles Kabeho ambaye pia alikuwa Waziri wa Elimu, katika Serikali ya Awamu ya Pili, iliyoongozwa na Mzee Ali Hassan Mwinyi.
Tangu wakati huo, Rostam amekuwa mwakilishi wa wananchi wa Igunga bungeni hadi jana alipotangaza rasmi kujiuzulu nafasi hiyo, akiwa amelitumika kwa miaka 18 na kuandika historia mpya katika siasa za Tanzania. Historia hiyo inatokana na ukweli kwamba, hakuna kumbukumbu zozote zinazoonyesha kuwa kuna mbunge yeyote aliyewahi kuachia ngazi nchini. Lakini kubwa zaidi ni mtindo alioutumia wa kuwaita wazee wa jimbo lake la Igunga na kuwaeleza uamuzi wake huo, ulioambatana na kujiuzulu na ujumbe wa halmashauri kuu ya Taifa ya CCM.
Rostam alirejea bungeni mwaka 1995 na baadaye 2005, jina lake lilipochomoza zaidi kutokana na jinsi alivyoshiriki katika mtandao uliomwezesha Rais Jakaya Kikwete kuingia madarakani. Kabla ya 2005, Rostam alikuwa akitajwa kuwa mmoja wa marafiki wakubwa wa Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa.
Siku zote, nafasi ya Rostam katika kundi la mtandao alikuwa akitajwa kuwa ‘mtu muhimu’.
Mafanikio anayojivunia
Mbali na kuwa mbunge wa kwa miaka 18, Rostam aliwahi kushika wadhifa wa Mtunza Hazina wa CCM, katika Sekretarieti ya kwanza ya CCM iliyoundwa na Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Rais Kikwete. Baadaye aliondoka katika nafasi hiyo katika mabadiliko yaliyomweka Amos Makalla kuwa Mtunza fedha wa chama hicho.
Pia Rostam kwa kipindi kirefu alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya CCM hadi alipojiuzulu Aprili mwaka huu, katika tukio lililohusisha kamati nzima kujiuzulu mjini Dodoma na hatimaye jana aliachia nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu (Nec).
Mwanasiasa huyo asiyependa kujitokeza hadharani na kuzungumza bungeni, anajivunia mafanikio mbalimbali aliyoyapata jimboni kwake katika kipindi cha miaka 18 ya ubunge wake uliokoma jana.Rostam alisema, wazee wa wa Igunga ndiyo waliompa heshima ya kuwa mbunge baada ya kukaa katika umoja wao na kumteua kuwa miongoni mwa vijana wa kuliwakilisha Jimbo la Igunga tangu mwaka 1994.
"Katika kipindi hicho chote cha utumishi wangu, nyinyi wazee wangu mmekuwa mhimili muhimu ambao umeniwezesha kutimiza wajibu wangu kwa bidii kubwa, maarifa na nidhamu ya hali ya juu, nikitambua namna ambavyo mmekuwa na imani kubwa juu yangu," anasema.
Miongoni mwa mafanikio makubwa anayojivunia kuyafikia kwa msaada wa wananchi na viongozi wa CCM Igunga ni kwamba, mwaka 1994 Igunga ilikuwa ni wilaya ya mwisho kwa maendeleo mkoani Tabora, lakini sasa inaongoza, imewekwa taa za barabarani, ina Bima ya Afya kwa kila kaya, zahanati kila kijiji na shule nyingi kuliko idadi ya kata zilizomo kwenye wilaya.
"Wazee wangu, nasema haya nikitambua kwamba, kama ilivyo katika maeneo mbalimbali hapa nchini, mafanikio makubwa tumeyapata katika nyanja za elimu, afya, makaazi bora na kilimo katika kipindi chote ambacho mmendelea kuniamini kuwa mbunge wenu kwa miaka 18 sasa," alisema.
Mwekezaji
Rostam ni mfanyabiashara, japokuwa biashara zake zimekuwa zikihojiwa sana. Katika miaka ya 1990, Rostam alianzisha kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) inayomiliki gazeti hili akishirikiana na Balozi Ferdinand Ruhinda, ambaye alikuwa mshirika mkubwa wa Rais Mstaafu wa Awamu ya tatu, Benjamin Mkapa.
Hata hivyo, baadaye Rostam aliuza hisa zake zote katika MCL na kujitoa kabisa na hadi sasa hana hisa, zaidi ya kubaki na heshima ya uasisi.
Makandokando yake
Pamoja na mafanikio ya kuwa na heshima ndani ya CCM, Rostam amejikuta akituhumiwa kuwa mmoja wa watu wanaojihusisha na ufisadi.
Mwanasiasa huyu ambaye kwa tabia yake ni nadra sana kusikika akizungumza, amekekuwa akitajwa katika tuhuma zisizo rasmi katika sakata la wizi wa fedha kupitia Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kupitia kampuni ya Kagoda Agriculture Ltd. Hata hivyo tuhuma hizo hazijawahi kuchunguzwa wala kuthibitika dhidi yake.
Rostam alidaiwa kuwa mhusika Kampuni ya Kagoda Agriculture iliyokwapua sh 40 bilioni, lakini ikabainika kuwa ni uongo.Hata hivyo, jana alipokuwa akitangaza kujiuzulu, aliweka wazi kwamba yeye ni mtu safi na kwamba hajawahi kushiriki katika vitendo vya rushwa.
Tuhuma hizo na nyingine ndizo ambazo zimefanya atajwe katika orodha ya watu ambao Sekretarieti mpya ya CCM imekuwa ikipigia debe mitaani kuwa ni mmoja wa wanaopaswa kujivua gamba.
0 comments:
Post a Comment