Social Icons

Saturday, July 23, 2011

GAZETI LA RAI LAPATA MSIBA MZITO

ALIYEKUWA Mhariri wa gazeti la Rai, ambaye pia ni Naibu Mhariri Mtendaji wa New Habari, Danny Mwakiteleko , amefariki dunia leo alfajiri katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Mwakiteleko alilazwa katika kitengo cha watu mahtuti Muhimbili baada ya ajali aliyoipata juzi usiku (jumatano) eneo la Tabata (ToT) na kukimbizwa katika Hospitali ya Amana, Ilala na baadaye Muhimbili.
Katika ajali hiyo gari alilokuwa akiendesha Mwakiteleko liligongwa na lori lenye trela, ambalo lilitoweka bila kujulikana saa nne usiku. Mwakiteleko alikuwa akitokea kazini Sinza ambako alifanya kazi hadi saa tatu usiku.

Mwakiteleko alipelekwa katika Hospitali ya Amana kwa uangalizi hadi saa 12 asubuhi, ambapo madaktari waliamua apelekwe Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Baada ya uchunguzi Muhimbili, madaktari walisema majeruhi alikuwa ameumia kichwani na kumfanya apoteze fahamu kiasi (semi-conscious) hivyo ikabidi apelekwe katika chumba cha upasuaji ambako madaktari walimhangaikia kuanzia saa sita hadi saa tisa mchana.

Jana Rais Jakaya Kikwete alienda kumuona na kuelezwa kwamba hali yake inaendelea vyema. BLOG hii inawapa pole wafiwa wote hasa familia ya Marehemu.
Danny Mwakiteleko (kulia) akiwa katika picha pamoja na wanachama wenzake wa Jukwaa la Wahariri pamoja na waandishi wa habari wa mkoani Arusha hivi karibuni.
Danny Mwakiteleko huenda hiki ndio kilikuwa cheti chake cha mwisho kupokea hapa duniani na aliyebahatika kumkabidhi cheti hicho ni Mkurugenzi wa Mahusiano wa Kampuni ya Bia Serengeti Teddy Mapunda.


Hii ilikuwa siku ya mwisho ya Mkutano wa Jukwaa la Wahariri mjini Arusha, Julai 16,2011.Wengine katika picha hiyo ni Mwenyekiti Absalom Kibanda (kushoto) Salim Said Salim na Neville Meena Katibu wa Jukwaa.

0 comments: