Na Saleh Ally
MSHAMBULIAJI wa Yanga, Davies Mwape amesema mabeki wanaompania wanapoteza muda kwa kuwa siku zote anataka kucheza katika kikosi kinachoshinda.
Akizungumza na Championi Jumatano, Mwape alisema kamwe huwa hakati tamaa wala kumhofia beki yeyote zaidi ya kuhakikisha anayemkaba ndiye anaingia hofu.
“Ukiniuliza mchezo upi ni mgumu zaidi katika niliyocheza siwezi kukuambia. Lakini mimi ni mshindani na ninataka kushinda kila ninapocheza, hata kama sijafunga.
“Najua mabeki wananipania sana lakini wanajisumbua tu kwa kuwa siwezi kuhofia chochote. Nimekumbana na walinzi wa kila aina na nimeweza kuwapa wakati mgumu,” alisema Mwape ambaye anazungumza taratibu.
“Sipendi kumhofia beki, huwezi kuniona nimecheza faulo ya kipuuzi. Lakini ninagombea mpira mwanzo hadi mwisho na ninatimiza kila nilichoelekezwa na kocha na pia akili ya ziada. Mshambuliaji unapaswa ucheze mechi mabeki wakikuhofia,” alisisitiza Mwape aliyejiunga na Yanga akitokea Konkola Blades ya Zambia.
Katika mechi dhidi ya Simba, Mwape alikuwa msumari wa moto kwa walinzi wa Simba, Kelvin Yondani na Juma Nyosso kutokana na kuwapa shughuli pevu hali iliyowafanya waanze kuonekana wana hofu kila Mzambia huyo anapokamata ‘gozi la ng’ombe’.
Mshambuliaji huyo aliangushwa na Nyosso na kusababisha penalti iliyoipa Yanga bao la kuongoza lililofungwa na Stephano Mwasika.
0 comments:
Post a Comment