Social Icons

Tuesday, September 13, 2011

LUNDENGA AOMBA RADHI KWA WALIOPATWA NA MAAFA YA AJALI YA MELI ZANZIBAR


USIKU wa kuamkia jumamosi ya tarehe 10 / 09/ 2011 tukio kubwa na la huzuni lilitokea huko Zanzibar ambapo wananchi wengi walipoteza maisha na wengine kujeruhiwa wakati walipopatwa na ajali ya kuzama kwa MELI iliyokuwa ikitoka Unguja kuelekea Pemba .
Kwa bahati mbaya siku hiyo ya Jumamosi taaasisi yetu ilikuwa inahitimisha Fainali za Taifa za Mashindano ya Urembo ya Miss Tanzania 2011.
Kama waandaaji wa Mashindano haya na wenye Mamlaka kamili ya maamuzi juu ya ama kuendelea au la kuahirisha jambo hili, tulipatwa na mshituko mkubwa sana juu ya tukio hilo .
kamati yetu ilikaa na kutakafari katika tukio hilo kwa kuzingatia mambo yafuatayo:-
· Taarifa kamili ya maafa haya tuliipata rasmi saa tisa na nusu mchana ( 9:30 ) siku ya jumamosi ambayo ilikuwa ni masaa machache kabla ya Fainali za Miss Tanzania kuanza katika ukumbi wa Mlimani City .
· Wenzetu wa TFF waliendelea na mechi za ligi kuu ikiwemo ya Yanga na Ruvu Shooting.
· Katika kumbi za starehe ikiwemo mabaa na burudani za muziki wa bendi na kumbi za disco ziliendelea kama kawaida.
· Muda uliokuwa umebaki kuwakilisha jina la mshiriki wetu kwenye fainali za Miss World zilikuwa zimekwisha hivyo kulikuwa na hatari ya kupoteza nafasi hiyo
· Pia tamko rasmi la kusimamisha shughuli zote za burudani lilianza tarehe 11 septemba 2011 kuomboleza Kitaifa maafa hayo.
Hata hivyo kama waandaaji tulifanya shindano tukiwa katika maombolezo kwani kabla ya kuanza shindano Watu wote waliokuwepo ukumbini walisimama kimya kwa dakika moja na hata washiriki walipoingia kwenye jukwaa kwa mara ya kwanza walikuwa wamevaa vitambaa vyeusi katika mikono yao ikiashilia maombolezo.
Hali hii imetupa mkanganyiko na kujikuta tukiendelea na mashindano kitu ambacho tunaona tumewakosea Watanzania wenzetu.
Kama Waandaaji tunapenda kusistiza kwamba tunawajibika kwa hayo yaliyotokea na si Taasisi yeyote au Kampuni yeyote na tunaomba ichukuliwe kama ni makosa ya kibinaadamu hasa ukizingatia mazingira magumu tuliyokuwa nayo kwa wakati huo na mkanganyiko wa matukio na taarifa za tatizo hilo.
KUOMBA RADHI
Hata hivyo shughuli hiyo inawezekana imewakwaza watu wengi na kwa sababu hiyo na pia hali halisi ya janga hilo na kwa niaba ya viongozi wenzangu na wadau wa shughuli zetu tunatoa tamko la dhati kwa Familia za ndugu wote walikumbwa na maafa haya, wale wote walionusurika katika ajali hii na Watanzania wote kwa ujumla, kwamba TUNAWAOMBA RADHI KWA MKANGANYIKO ULIOTUTOKEA HADI KUFIKIA HALI HII. Hatuna neno zaidi ya kusema na kusisitiza “TUNAOMBA RADHI”
Mwenyezi MUNGU aziweke roho za marehemu mahali pema peponi,
Amina,
Hashim Lundenga
Mkurugenzi

0 comments: