Social Icons

Tuesday, April 5, 2011

HATARI: USIMLISHE MWANAO MAZIWA YA SOYA!


Ni kawaida kutokea mtoto mchanga akakataa kunyonya maziwa ya mama, badala yake akapewa maziwa ya ng’ombe, mbuzi au maziwa yatokanayo na soya. Hali hii hutokea pale mtoto anaponyonya maziwa ya mama na kuanza kuumwa tumbo au kuharisha.

Hali hii inapotokea, wazazi wengi hukimbilia kwenye maziwa ya kopo (Milk Formular), wachache kwenye maziwa ya ng’ombe au mbuzi. Maziwa ya kopo yana orodha ndefu na miongoni mwa orodha hiyo yamo yale yanayotengenezwa kutokana na soya au kwa jina lingine yanajulikana kama Soy Formula au Soy Milk.

Maziwa ya soya yameonekana kuwa na madhara makubwa kwa mtoto kuliko faida, licha ya matangazo na propaganda za kibiashara zinatolewa kuwahimiza watu utumiaji wake kama chakula bora. Madhara hayo huwapata watumiaji kuanzia utotoni hadi ukubwani.

KWA NINI MAZIWA YA SOYA HAYAFAI?
Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti wa Bi. Claire McCarthy wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Havard, ni watoto wachache sana wanaonufaika na maziwa ya soya lakini wengi huathirika kutokana na kunywa maziwa yaliyotokana na soya iliyoandaliwa isivyotakiwa.

Ili kuonesha ukubwa wa madhara ya maziwa ya soya kwa watoto, imeelezwa na watafiti kwamba mtoto anayepewa maziwa hayo ni sawa na kumpa vidonge vitano vya mpango wa uzazi (contraceptive pills) kila siku, ikitegemea na kiwango unachompa na kama mtoto ni mnywaji mzuri wa maziwa hayo!

HII INA MAANA GANI?
Athari za kiafya anazoweza kuzipata mtoto huyu anayeingiza kiasi kingi kama hicho cha homoni katika mwili wake mdogo kila siku ni pamoja na hizi zifuatazo:

-Kuwa na mzio (Allergy) na vyakula na matatizo katika mfumo wa usagaji wa chakula,
-Kuwa na matatizo ya kitabia,
-Kupatwa na ugonjwa wa pumu
-Kubalehe mapema (kwa wavulana) na kuvunja ungo mapema na kutokupata siku zao (kwa wasichana)
-Hatari ya kupatwa na ugonjwa wa saratani, na ukubwani kupatwa na uvimbe kwenye njia ya mkojo na uzazi.
Kwa ujumla, maziwa yanayotengenezwa kutokana na soya hayafai kumpa mtoto na asitokee mtu akakudanganya kuwa ni bora kuliko maziwa ya mama au ya ng’ombe.

SOYA INA FAIDA, LAKINI…
Yale maelezo kuwa soya ina virutubisho muhimu kwa afya ya binadamu, kama vile kutoa kinga dhidi ya magonjwa ya moyo, saratani ya kibofu, ini na figo, ni ya kweli lakini kwa soya iliyoandaliwa inavyotakiwa tu.

Utaweza kupata faida za unga wa soya na bidhaa zake iwapo utaiandaa kama inavyotakiwa. Ili kupata bidhaa bora za soya, iwe yenyewe ya kupika kama mboga au unga wake, ni lazima uiloweke kwa siku mbili na ‘uivundike’ ili kuondoa kabisa ngozi yake ya juu.
Uandaaji wa soya unahitaji mafunzo maalum na siyo kila mtu anaweza kuiandaa, kuila na kupata faida zake. Hivyo ili kupata faida za soya kama zilivyoelezwa hapo juu, lazima utumie soya iliyovundikwa (fermented soy).

Mchakato wa kuandaa soya ni pamoja na kuiloweka kwa muda usiopungua siku 2, kisha kuiosha kwa maji zaidi ya mara 10 na baada ya hapo kuihifadhi kwa muda wa siku mbili kabla ya kuamua kuipika kama mboga au kuianika na kusaga unga wake. Mchakato huo utakuwezesha kutoa maganda yote ya nje ya soya na hivyo kuondoa chembe zote zenye madhara.

Naamini kwamba wasomaji wa makala haya mnajali sana suala la afya zenu pamoja na watoto wenu. Hivyo nawahimiza kuendelea kutafiti na kujifunza ukweli kuhusu unga wa soya tunaouziwa madukani kama umeandaliwa inavyotakiwa, vinginevyo huna sababu ya kuamini soya ni chakula bora kwa afya yako na badala yake iepuke.

0 comments: