Social Icons

Wednesday, March 9, 2011

SITTA: DOLA ISITUMIKE DHIDI YA CHADEMA

Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta.

WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta ameishauri Serikali isitumie vyombo vya dola kuzima moto wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutokana na kauli zao za uchochezi.

Kauli hiyo inapingana na msimamo wa CCM uliotolewa hivi karibuni na Katibu wa Halmashauri Kuu ya chama hicho, Itikadi na Uenezi, John Chiligati ulioitaka serikali na vyombo vya dola kuchukua hatua dhidi ya viongozi wakuu wa Chadema kwa kuwa, wanachochea uasi dhidi ya serikali iliyopo madarakani.

Sitta amesema hayo siku nne tu baada ya Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya tatu, Frederick Sumaye kukitaka CCM kukabiliana na hoja za Chadema kisiasa badala ya kuiachia serikali ipambane nao akisema kazi ya siasa ni ya chama na si serikali. Hivyo kinapaswa kuwa mstari wa mbele kupambana na Chadema kwa sera na kujibu hoja zao zote ili kuongeza imani ya wananchi kwa chama hicho.

“Wale (Chadema) wanafanya kazi za siasa na hawa (CCM) wamekaa kimya, wanaiachia serikali ndiyo inatoa majibu, hali hiyo si nzuri. Chama kinapaswa kujibu hoja zote na kama hakina majibu, kiombe kwa serikali,” alisema Sumaye.

Akizungumza wakati wa mapumziko kwenye mkutano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unaofanyika jijini hapa, Sitta alisema kuwa Serikali inatakiwa kutambua kuwa vyama vya upinzani vipo na vimejiimarisha kutaka kuing'oa serikali hii na kwamba ndani yake kuna viongozi ambao wanakubalika kwa wananchi.

"Kutokana na uimara walionao, Serikali isitegemee kwamba wapinzani wataongea lugha nyepesi juu yake na viongozi wake na wala tusitegemee kuwa wapinzani ni rafiki zetu watatuonea huruma. Kinachotakiwa ni kujirekebisha haraka na kuwa wepesi wa kukubaliana na mambo," alisema Sitta.

Lakini alisema Serikali inatakiwa kuchukua hatua mapema katika jambo lolote linalokwenda kinyume na taratibu badala ya kukaa muda mrefu na kuwaingiza wananchi katika wasiwasi.Sitta alisema kuwa viongozi waliopo madarakani wanatakiwa kujitazama na kuachana na tabia ya kutumia vyeo vyao kuendeleza biashara zao jambo ambalo hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alilikemea na kuwataka watu wote kuwa sawa.

"Mimi binafsi nashangaa kiongozi ambaye ni mbunge ni mfanyabiashara mkubwa mwenye biashara kubwa sana anapata wapi muda wa kufanyabiashara hiyo kama siyo kutumia madaraka yake katika kuendeleza biashara hizo?" Alihoji Sitta. Alisema kuwa wananchi wana macho na wanaona chama hakifai kutokana na viongozi kutumia madaraka kujinufaisha wenyewe na kwamba hiyo ndiyo inayochafua mazuri ya CCM.

Anaamini kuwa wakati umefika kwa chama kuchukua hatua kama Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete alivyobainisha awali kwa kuwa hakiwezi kuyaacha mazuri ya CCM yakayeyuka pasipo sababu. "Naamini viongozi wa katika ngazi ya Taifa watahakikisha amani inakuwapo ndani ya chama. Bado tuna mashabiki wengi wanaokipenda chama ila wanakwazika pindi wanapoona kunakuwapo na ucheleweshwaji wa kuchukua hatua," alisema Sitta.

Akizungumzia vuguvugu la siasa nchini, Sitta aliwataka wapinzani wasitumie ukame unaolikabili taifa kuwahadaa wananchi kwa sababu, hali hiyo inaweza kuikumba serikali ya nchi na chama chochote duniani na kwamba hii iliyopo madarakani, haipaswi kubebeshwa lawama.

Alisema kuwa si busara kwa wapinzani kuhubiri habari za kumwaga damu na kuwataka wananchi kulinganisha wapinzani na serikali iliyopo madarakani kwa kuhoji kama itaweza kuwa serikali mbadala badala ya CCM.

Alisisitiza kwamba CCM ina hazina kubwa ya viongozi ambao wanaweza kuendesha nchi hii na kudai kuwa, wanachama wa chama hicho tawala wana nafasi ya kuwaondoa viongozi wabovu kwenye uchaguzi ndani ya chama utakaofanyika mwaka 2012.

Mjadala wa uhalali wa mikutano na maandamano ya Chadema uliibuliwa na Rais Jakaya Kikwete alipolieleza taifa kuwa, chama hicho cha upinzani kina lengo la kuleta machafuko nchini. Rais Kikwete alisema hayo alipokuwa akilihutubia taifa mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu kupitia redio na televisheni.

Kauli hiyo ya Rais Kikwete ambaye Chadema waliipuuza, ilisisitizwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira aliyeonya kuwa Chadema kisije kuilaumu serikali ikikosa uvumulivu na kuanza kutumia dola kukishughulikia.


CHANZO: MWANANCHI MACHI 9, 2011

0 comments: