Social Icons

Wednesday, March 16, 2011

KOCHA PHIRI: HATUTALINDA LANGO LETU DRC CONGO

Na Phillip Nkini
KOCHA Mkuu wa Simba, Patrick Phiri, amesema hajawandaa vijana wake kwenda DR Congo kulinda lango bali watacheza na kuonyesha kiwango ili kupata matokeo mazuri.

Simba inatarajiwa kwenda nchini DR Congo kuvaana na TP Mazembe ya huko kwenye mchezo wa hatua ya kwanza wa Klabu Bingwa Afrika utakaopigwa wikiendi ijayo kwenye Uwanja wa De La Kenya.

Akizungumza na Championi kutoka mkoani Arusha ambapo timu hiyo imeweka kambi, Phiri alisema kuwa, wanakwenda Congo kwa tahadhari kubwa lakini kamwe hawana mpango wa ‘kupaki basi’ langoni mwao.

“Ndiyo tumemaliza mazoezi sasa hivi, tumerejea hotelini kwa ajili ya mapumziko. Tunashukuru kwa kuwa tumefanya mazoezi kwenye mazingira mazuri na tulivu.

“Ingawa tuna wachezaji wawili majeruhi, Emmanuel Okwi na Patrick Ochan, watu hao hawana majeraha ya kutisha sana. Okwi ana maumivu kidogo, lakini Ochan yeye anasumbuliwa na mafua na wameshachukuliwa na kupelekwa hospitalini, tunaamini watakuwa fiti kwenye mchezo wetu ujao.

“Tunakwenda kupambambana na Mazembe huku kila mmoja akiwa na ari ya hali ya juu, ukweli ni kwamba tunakwenda pale kutafuta matokeo mazuri na wala hatuna mpango wa kulinda lango,” alisema Phiri aliyeipa Simba ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom msimu uliopita bila kufungwa na kuongeza kuwa:

“Hakuna anayejua nini kitakachotokea, lakini hatuna hofu hata kidogo na ukweli ni kwamba tutamshangaza kila mmoja baada ya mchezo huo,” alisema Phiri ambaye timu yake inashikilia usukani wa Ligi Kuu ya Vodacom.

Mazembe ndiyo bingwa mtetezi wa Klabu Bingwa Afrika, lakini ina rekodi ya kuwa timu ya kwanza ya Afrika kufika fainali ya Klabu Bingwa Dunia ilipochapwa mabao 3-0 na Inter Milan mwishoni mwa mwaka jana.

0 comments: