HATIMAYE Serikali imesalimu amri kwa kukubali kulipa fidia ya Sh 185 bilioni kwa kampuni ya kufua umeme wa dharua ya Dowans Tanzania Ltd, huku Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema akisema kuwa "mjadala kuhusu suala hilo umefungwa rasmi".
Ulipaji wa fidia hiyo unafuatia uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara (ICC Court), Novemba 15, mwaka huu chini ya Mwenyekiti Gerald Aksen na wasuluhihi Swithin Munyantwali, Jonathan Parker uliamuru Tanesco iilipe Dowans kiasi hicho cha fedha.
"Jopo la wasuluhishi limeamuru zaidi ya Sh36bilioni (dola za Marekani 24,168,343) na riba ya asilimia 7.5 kwa mwaka inayofikia kiasi cha zaidi ya Sh 26bilioni (dola za Marekani 19,995,626) tangu Juni 15, 2010 hadi fidia hiyo itakapolipwa,’ ilieleza sehemu ya uamuzi huo.
Pia jopo hilo la wasuluhishi wa migogoro ya kibiashara liliamuru Sh60bilioni (sawa na dola za Kimarekani 39,935,765) na riba ya kiasi cha asilimia 7.5 ambayo ni sawa na Sh 55bilioni (dola za Marekani 36,705,013.94) zilipwe kuanzia Juni 15, 2010 hadi wakati wa malipo.
Jopo hilo lilisisitiza kuwa ada na gharama za wasuluhishi na za utawala Sh1bilioni (dola za Marekani 750,000) kwa wasuluhishi wa ICC zinatakiwa zilipwe na pande zote husika yaani Tanesco na Dowans.
"Tanesco wanatakiwa kumlipa mdai (mlalamikaji) Sh3bilioni (dola 1,708, 521) ikiwa ni gharama za uendeshaji wa kesi na gharama zingine na kwamba madai mengine yaliyotolewa na pande zote katika kesi hiyo yanatupwa.
Awali baada ya uamuzi huo kufikiwa, Tanesco ilionyesha nia kwamba ingechukua hatua za kukata rufaa, lakini Jaji Werema aliliambia Mwananchi jana katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam kuwa hakuna haja ya suala hilo kukatiwa rufaa, hivyo kuyeyusha ndoto hizo za Tanesco.
Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, William Mhando katika mkutano wake na wahariri wa vyombo vya habari wiki mbili zilizopita alisema shirika lake lingeweza kutoa tamko kuhusu hatua za kuchukua kuhusu uamuzi wa ICC, lakani akaweka wazi kuwa walikuwa wakisubiri uamuzi huo kusajiliwa rasmi katika Mahakama Kuu nchini.
Hata hivyo, kutokana na kauli ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, sasa ni rasmi kwamba hakutakuwa na hatua zozote za kisheria dhidi ya uamuzi wa ICC na badala yake Tanesco watatakiwa kujipanga kuwalipa Dowans mabilioni hayo ya shilingi kama walivyoamriwa.
Taarifa za ndani ya Tanesco, zinasema kwamba shirika hilo limeanza kuweka fedha kwa ajili ya malipo katika benki moja (jina tunalihifadhi kwa sasa) jijini Dar es Salaam
Akizungumza na Mwananchi baada ya hafla ya kuapishwa kwa Jaji Mkuu mpya, Mohamed Chande Othman jana, Jaji Werema alisema ameshamaliza kuisoma hukumu hiyo na kufanya uamuzi ambao tayari ameukabidhi kwa Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja kwa ajili ya hatua nyingine baada ya kuridhika nayo.
“Mimi kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali nimeisoma hukumu hiyo kwa makini na nimeridhika nayo kuwa iko sawa,” alisema Jaji Werema.
Alisema kwa maana hiyo, haoni haja ya kukata rufaa na kwamba licha ya kusikia baadhi ya watu wakijigamba kwamba wakipewa kesi hiyo wanaweza kushinda, amewaambia mawakili wa serikali kwamba asingependa kusikia uwepo wa mpango wowote wa kukodi mawakili kwa lengo la kuendelea na kesi hiyo.
“Kwa hukumu hii siwezi kusema tutalivalia njuga suala la Dowans maana kwa hukumu hii hata ukiivalia hiyo njuga itafikia mahalai njuga hizo zitakatika tu,” alisisitiza Jaji Werema.
Kauli ya Jaji Werema imekuja wakati wanaharakati, wananchi wa kawaida na baadhi ya viongozi wa serikali wakipinga waziwazi hukumu hiyo akiwemo Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta aliyekaririwa na baadhi ya vyombo vya habari akisema kuwa kuilipa fidia Dowans "ni kuhujumu uchumi wa nchi".
Sitta ambaye alikuwa Spika wa Bunge la Tisa akiongoza vita dhidi ya ufisadi alikwenda mbali zaidi na kudai kwamba kuilipa Dowans ni mbinu chafu za watuhumiwa wa ufisadi ambao bado wana ajenda za kuingia Ikulu mwaka 2015.
Hata hivyo, katika mazungumzo yake jana, Jaji Werema alisema kwa mtu yeyote makini hawezi kupinga hukumu hiyo kwani mfumo wa uamuzi unaotumiwa na ICC hauwezi kutoa fursa ya kuwepo chochote cha kupinga.
Alisema wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo pande zote, yaani Tanesco na Dowans walimchagua msuluhishi wake na kwamba baada ya wasuluhishi hao kutoa uamuzi, ulipelekwa katika mahakama hiyo kwa ajili ya kuupitia na kuuthibisha.
Kuhusu hoja kwamba huenda upande mmoja ulitumia mbinu chafu katika kupata ushindi, Jaji Werema alisema msuluhishi anayeteuliwa na pande zinazohusika katika kesi si wakili wa upande wowote na kwamba jukumu lake ni kuangalia suala zima tu jinsi lilivyo na kutoa uamuzi wa haki.
“Hata unapomteua mtu kuwa ‘Arbitrator’ (msuluhisi) si wakili wako, hivyo unaweza kumkataa. Kuna taratibu za kumkaba, lakini huwezi kumkataa kwa sababu hafuati mambo yako bali kama hafuati ‘ethics’ (maadili ya kazi),” alisema Jaji Werema na kuongeza;
“Kwanza arbitrator hapaswi kujua mambo yako na hupaswi kumweleza, hivyo upande mmoja ukijua kuwa umemweleza mambo yako una haki ya kumkataa,”.
Mwanasheria huyo Mkuu wa Serikali alieleza kushangazwa na kejeli na malalamiko yanayotolewa na watu mbalimbali juu ya uamuzi huo akidai kuwa hao wanaopiga kelele sasa wakipinga uamuzi huo ndio baadhi yao walikuwa wakipiga kelele kuishinikiza serikali kuvunja mkataba na Dowans.
Jaji huyo alisema kuwa kuna upotoshaji katika hukumu hiyo akidai kuwa kuna mambo mengine ambayo yamekuwa yakisemwa katika hukumu hiyo jinsi isivyo sahihi.
“Watu wamezungumza sana, nendeni mkaisome muone ile Dowans ni ya nani na imesajiliwa wapi, maana watu walitaka kupotosha kidogo,” alisema Jaji Werema.
Ingawa hakuweza kuainisha aina ya upotoshaji huo, lakini Jaji huyo alisema kwa mujibu wa rekodi, Dowans ilisajiliwa Costa Rica na kwamba inaonesha kuwa Rostama Aziz (Mbunge wa Igunga) alipewa nguvu ya kisheria tu.
Hivyo alitoa wito kwa Watanzania wote wanaoweza wausome kwanza uamuzi huo ili kuweza kujua hasa mfumo uliotumika katika usuluhishi, hadi kufikiwa kwa uamuzi wa Dowans kupewa haki ya kulipwa.
Tanesco inabeba mzigo wa kulipa gharama hizo wakati ambao nchi imekumbwa na mgawo wa umme untokana na kasoro mbalimbali katika mitambo ya kuzalishia nishati hiyo, sambamba na uamuzi wa kupandishwa kwa gharama za umeme ambao umelalamikiwa na wananchi.
CHANZO: MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment