Social Icons

Tuesday, October 26, 2010

TARIQ AZIZ: MSAIDIZI WA SADDAM HUSSEIN AHUKUMIWA KUNYONGWA


Tariq Aziz.

Baghdad, Iraq
ALIYEKUWA msaidizi mkuu wa kimataifa wa utawala wa Saddam Hussein nchini Iraq, Tariq Aziz, leo amehukumiwa kunyongwa kwa ajili ya kuendesha manyanyaso dhidi ya waumini wa madhehebu ya Shia nchini humo Tukio hilo limekuja baada ya miezi mitatu tu baada ya Wamarekani kumsalimisha mtu huyo kwa serikali ya Iraq.
Msemaji wa Mahakama Kuu ya Iraq, Mohammed Abdul-Sahib, hakutaja ni wapi mtu huyo mwenye umri wa miaka 74 ambaye aliwahi kuwa waziri wa mambo ya nchi za nje angenyongewa. Hata hivyo, Aziz amepewa siku 30 za kukata rufaa.
Aziz, ambaye alikuwa Mkristo pekee miongoni mwa washirika wakuu wa Saddam ambaye alikuwa mfuasi wa madhehebu ya Sunni, alikuwa amevaa suti ya bluu wakati akiwa amekaa peke yake mahakamani akiwa ameinama.
Mwanasheria wake kutoka Jordan, Badee Izzat Aref, aliishutumu serikali kwa kumbambikia tuhuma hizo ili kupotosha nadhari ya umma kuhusu kufichuliwa hivi karibuni kwa manyanyaso wanayofanyiwa wafungwa na majeshi ya Iraq kwa mujibu wa hati za jeshi la Marekani zilizotolewa wiki iliyopita na taasisi ya WikiLeaks.
“Tunalijadili suala hili na hatua za kuchukua,” Aref aliliambia shirika la habari la The Associated Press mjini Amman, nji mkuu wa Jordanian na kuongeza kwamba "hukumu hii si ya haki na ilikuwa na madhumuni ya kisiasa."
Azizi alifahamika kimataifa kama mtetezi wa utawala wa Saddam nchini humo na mpinzani mkuu wa Marekani hususani alipokuwa waziri wa mambo ya nje baada ya uvamizi wa Iraq nchini Kuwait mwaka 1990 na baadaye kuwa makamu wa waziri mkuu. Mkutano wake na aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani, James A. Baker, mjini Geneva, Januari 1991 ulishindwa kuzuia kuzuka kwa Vita vya Ghuba.
Azizi pia alikutana na Papa John Paul wa Pili huko Vatican wiki kadhaa kabla ya uvamizi ulioongozwa na Marekani mnamo Machi 2003, katika juhudi zake za kuepusha vita hivyo.

0 comments: