Social Icons

Wednesday, January 4, 2012

NUKUU YA LEO

“Gezaulole baba, Gezaulole mama ee,
Twendeni Kibugumo na Mwanadilato kwenye makao mapya,
Gezaulole baba, Geza ulole mama eee!”
Ndugu zangu,
Hapa nanukuu gazeti la Mwananchi leo Jumatano; “Majuzi, Dk Magufuli alifanya ziara ya ghafla katika eneo la vivuko hivyo na kuwaambia wananchi waliomzomea kwamba kama wakishindwa kulipa nauli hiyo ya Sh200 ni vyema wakapiga mbizi baharini au kuzunguka Kongowe kuingia katikati ya jiji au warudi vijijini wakalime.”- Mwisho wa kunukuu.
Utotoni katika Dar es Salaam hii, nilishuhudia kwa macho yangu msako wa wazururaji. Niliona jinsi mgambo wa jiji walivyokuwa wakiwadhalilisha vijana na watu wazima kwa kuwakamata, kuwafunga mashati na kuwapandisha kwenye malori tayari kwa safari za kwenda Gezaulole. Kosa lao, walikuwa wakizurura mijini bila kazi. Hivi, anayetafuta kazi atabaki nyumbani kuisubiri, si ni lazima apige mguu kuitafuta? Sijui leo ungefanyika msako wa wazururaji Dar yangehitajika malori mangapi?
Na miaka ile ya sabini tulipokuwa watoto tulisikia hata nyimbo za redioni kuhimiza ‘ wazururaji’ waende kwenye vijiji vipya vilivyoandaliwa na Serikali kama makazi ya ‘ Wazururaji’. Watoto wa enzi hizo huenda tunakumbuka wimbo huu;
“ Gezaulole baba, Gezaulole mama ee,
Twendeni Kibugumo na Mwanadilato kwenye makao mapya,
Gezaulole baba, Geza ulole mama eee!”

Kigamboni ya enzi hizo ilikuwa shamba kweli. Wengi wa waliofikishwa huko Gezaulole na vijiji vingine kule Kigamboni wakayaanza maisha mapya ya vijijini. Kuna waliokimbia Gezaulole wakarudi tena mjini au kwenye vijiji vyao vya asili. Kuna waliobaki huko Gezaulole, wakafyeka mapori yao. Wakaanza kilimo, . Wakaizoea hali mpya. Wakajenga familia zao huko.

Ajabu, leo wenye fedha ndio wanaokwenda kuyanunua kwa bei ya hadaa, maeneo ya watoto na wajukuu wa ‘ wazururaji’ wa enzi za Mwalimu. Kuna watoto na wajukuu wa ‘wazururaji’ waliobaki na vieneo vidogo. Miongoni mwao ndio hao wanaofanya shughuli za kusukuma mikokoteni na kuendesha maguta.

Ndio hao, waliokisikia kilio cha kutaka uwepo wa pantoni ya uhakika kwa miaka nenda , miaka rudi. Wamesikia kilio cha kujengewa daraja pia na ahadi zake. Na sasa wanaongezewa nauli ya kivuko kwenda na kurudi mjini.
Ni hivi; mkazi wa Magomeni hata kama hana nauli anaweza kutembea kwa miguu kukatisha Jangwani na akamwona mgonjwa wake Muhimbili, au kwenda kuhangaikia kibarua Kariakoo. Na jioni ikifika, hata kama hana nauli ya Daladala, atakatisha Jangwani na kufika Magomeni kwenye chumba chake cha kupanga.

Lakini, mkazi wa Kigamboni kama hana nauli ya mia tatu ya pantoni na kama anataka kuvuka kwenda kumwona mgonjwa wake Muhimbili au kuhangaikia kibarua Kariakoo ana mawili, kwa mujibu wa Magufuli; ama apige mbizi au azungukie Kongowe, kwa miguu, mwendo wa nusu siku kama si siku nzima. Na hapa ndipo ilipo hoja ya msingi ya kumfikiria mtu wa kawaida wa Kigamboni, Gezaulole na kwingineko ng’ambo ya pili ya bahari.

Vinginevyo, kwa kusema kuwa asiye na nauli arudi kijijini akalime ina maana pia, kuwa kuishi Jangwani, Mburahati na Mabibo kunaweza kuwa na nafuu zaidi kwa mtu wa Kigamboni mwenye hali ngumu kiuchumi. Kwamba hatimaye tunawaambia watoto na wajukuu wa ‘ wazururaji’ wa enzi za Mwalimu; “Rudini mjini’. Na wimbo ule leo labda ungeimbwa hivi;

“ Mburahati mama, Mburahati baba ee,
Rudini Jangwani, na Mwananyamala kwenye maisha bora!”
Haki ya Mungu!

Maggid Mjengwa,
Msamvu, Morogoro.


0 comments: