MADIWANI FUATILIENI MIRADI YA MAENDELEO
Na Gladness Mushi, ARUSHA
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Bw. Magesa Mulongo,amesema kuwa kama madiwani kutoka katika kata zote watashiriki katika kusimamia miradi mbalimbali ya maendeleo ya vijiji na kata basi miradi hiyo itaweza kujengwa katika viwango vya hali ya juu sana na pia itaweza kuwanufaisha zaidi wananchi ambao ndio walengwa wa miradi hiyo.
Bw Magesa aliyasema hayo hivi karibuni mkoani Arusha wakati akiongea na viongozi mbalimbali wa serikali za mitaa kuhusu masuala na mikakati mbalimbali ya kimaendeleo kwa Mkoa wa Arusha.
Amesema,ili miradi iboreshwe kwa kiwango ambacho kinakubalika ni lazima kuwe na mipango mahususi kwa viongozi wa serikali hizo hasa Madiwani ambapo wanatakiwa kuhakikisha kuwa wanakuwa wasimamizi wazuri wa miradi ambayo inalenga kutoa huduma kwa jamii.
Alisema kwa utaratibu huo wa kufuatilia na kukagua mara kwa mara shuguli za miradi hiyo ya maendeleo katika ngazi ya kata unawezekana kufanyika na kuwa na manufaa kwa wananchi ambapo ufuatiliaji huo unaweza kuungwa mkono hata na ngazi ya halmashauri.
Alibainisha kuwa ni wazi miradi mbalimbali katika ngazi za kata,Vijiji,zinashindwa kukamilika na kuwafikia watumiaji ambao ndio waliolengwa, kwa kuwa bado baadhi ya watendaji wanashindwa kufuatilia kwa ukaribu miradi hiyo hali ambayo inasababisha hasara kubwa sana kwa Serikali, na Wahisani mbalimbali.
“Nawasihi sana Madiwani hakikisheni kuwa mnajua na kufuatalia miradi yote ambayo imo kule kwenye kata zenu hata kama miradi hiyo si ya Serikali kwa kuwa malengo halisi ya miradi hiyo ni kumkomboa Mtanzania”alisema bw Magesa.
Akizungumzia suala la usimamizi wa Fedha alisema kuwa nao maafisa mipango wanatakiwa kuhakikisha na kukagua ubora wa mradi kabla hawajapitisha malipo mbalimbali kwa ajili ya miradi hiyo kwa kuwa baadhi ya miradi inapitishwa na halmashauri wakati miradi hiyo haina ubora uliokusudiwa.
“Eti unakuta mkuu wa idara anakaa ofisini alafu anapitisha malipo
kwa ajili ya miradi wakati hajui hata mradi ulipo,wala ubora wake sasa watu wa hali hii mimi sitawaacha kabisa na badala yake nawasihi sana madiwani kuwa hakikisheni kabla hamjapitisha mradi mnashirikiaana na halmashauri zenu hata kwa njia ya ushauri wa wataalamu wake’aliongeza Bw Magesa.
Aliwataka wakuu wa idara kuhakikisha kuwa wanashirikiana na uongozi mbalimbali wa serikali za vijiji katika kuboresha na kuimarisha miradi ya Serikali pamoja na Miradi ya wahisani ili kuharakisha maendeleo kwa walengwa hasa katika maeneo ya vijijini.
Habari/Picha: Fullshangwe Blog
0 comments:
Post a Comment