Social Icons

Wednesday, September 14, 2011

HADI LEO HII JUMLA YA MAITI 202 ZILIZOPATIKANA KUFUATIA AJALI YA MELI MV SPICE ISLANDER ILIYOTOKEA HIVI KARIBUNI

Jumla ya maiti 202 tayari zimepatikana katika ajali ya Meli ya Mv.Spice Islander iliyotokea hivi karibuni huko Nungwi hadi hapo jana.

Maiti tano zaidi zilipatikana hapo jana sehemu ya Shimoni Mombasa Kenya ambapo maiti zote hizo zilizikwa huko huko Kenya kutokana na hali ya maiti zilivyo ambapo kabla ya jana maiti 197 zilikuwa zimepatikana.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Mohammed Aboud Mohammed zilieleza kuwa aliwasiliana na Balozi mdogo wa Tanzania Nchini Kenya na kumthibitishia kwamba isingewezekana kuwasafirisha maiti hao kuwaleta Zanzibar kwa ajili ya kutambuliwa na jamaa zao kutokana na hali ilivyokuwa.

Amesema maiti hao mmoja inakadiriwa ni miaka minane, mwengine miaka 20 hadi 25 na wengine miaka 40 wote ni wanaume na mtoto mchanga mwanamke anakadiriwa na umri wa mwaka mmoja na nusu ambao wamepatikana katika kijiji cha Diani.

Kazi ya uokoaji bado inaendelea kwa ushirikiano mkubwa wa vikosi vya ulinzi na usalama, raia wa Tanzania pamoja na kikosi maalum cha Uokozi kutoka Afrika ya Kusini.

Wakati huo huo michango ya Rambi rambi inaendelea ambapo hapo jana Isnaashir imetoa jumla ya Shl. Milion 30, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wametoa shl. Milion 15 Wabunge wa Afrika Mashariki wamechangia Milion 2 na Benki ya NMB imekabidhi hundi ya Milion 20.

Fedha zote hizo zimekabidhiwa kwa Mwenyekiti wa Kamati ya maafa ya kitaifa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd ambaye pia ni Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Shughuli za uchangiaji bado zinaendelea na wananchi pamoja na Taasisi mabalimbali za binafsi na Serikali zinaendelea kutoa michango yao.

0 comments: