Social Icons

Monday, February 7, 2011

KIGOGO WA CCM KUHAMIA CCK!

Mwenyekiti wa CCK, Costantine Akitanda akitangaza ujio wa kigogo wa CCM katika chama chake.

CHAMA Cha Kijamii (CCK) ambacho ni chama cha siasa kilichoundwa na baadhi ya waliokuwa viongozi wa chama cha CCJ baada ya chama hicho kufa, wamedai kigogo mmoja wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ameomba kujiunga na chama hicho ambapo wanatarajia kumtangaza hivi karibuni baada ya kukamilisha utaratibu wa kukihama CCM. Mwenyekiti wa chama hicho, Costantine Akitanda, amesema hayo leo katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Jijini Dar es Salaam.

MISRI WAANZA MAONGEZI



Waandamanaji wakimiminika kwenye uwanja wa Tahrir, Cairo


Baada ya wiki mbili za maandamano ya kuipinga serikali nchini Misri, makamu wa Rais Omar Suleiman ameanza mazungumzo na makundi ya upinzani.


Miongoni mwa wanaoshiriki kwenye mazungumzo hayo ni lile la Muslim Brotherhood na waakilishi wa vijana, ambao ndio wamekuwa wakiongoza maandamano.

Taarifa zinasema tayari makubaliano yamefanyika ya kuunda kamati ya kuchunguza mabadiliko yanayotakiwa kufanyika katika katiba ya nchi hiyo.

Kundi la Muslim Brotherhood ambalo bado limepigwa marufuku nchini Misri lilikuwa limesema linasubiri kuona ikiwa serikali iko tayari kufanya mabadiliko ya kisiasa mara moja.

Bado linamtaka Rais Mubarak ajiuzulu, na linasema ni sharti serikali ya muungano iundwe, na pia sheria za dharura zibadilishwe.

Hii ni mara ya kwanza kwa serikali ya Misri kufanya mazungumzo na kundi hilo la Muslim Brotherhood lililopigwa marufuku.

Makundi ya upinzani yanataka Bw Mubarak kujiuzulu mara moja lakini amesema kuondoka kwake kwa dharura kutaleta vurugu.

Aidha, amesema hatagombea kiti cha urais katika uchaguzi utakaofanyika mwezi Septemba.

Wakati huo huo, benki zilizokuwa zimefungwa kwa zaidi ya juma moja zimefunguliwa huku kukiwa na wasi wasi kwamba watu wengi watatoa pesa zao kutoka benki kufikia kiwango kikubwa mno.
Raia wantoa pesa kutoka benki

Raia wantoa pesa kutoka benki

Uchumi wa Misri umeumia kutokana na maandamano dhidi ya Rais Mubarak, na serikali ina hamu ya kuona nchi ikirudi katika hali ya kawaida.

Halaiki ya watu wamekuwa wakiandamana katika mitaa ya Cairo na miji mingine majuma mawili yaliyopita wakitaka mabadiliko katika mfumo wa demokrasia.

Kabla ya mazungumzo msemaji wa Muslim Brotherhood, Mahmoud Azzat, alisema wakuu wameanza kukubali shuruti zao.

Lakini maandamano yanaendelea leo katika medani Tahrir mjini Cairo.(BBC Swahili)

HOTUBA YA JK DODOMA TAFASILI YANGU



Ndugu Zangu,

JUMAMOSI nimemsikiliza Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete. Mwenyekiti Kikwete alikuwa akihutubia kule Dodoma katika kuadhimisha miaka 34 ya kuzaliwa kwa Chama chake Cha Mapinduzi.
Ukweli kwamba CCM ndio chama tawala ndio wenye kutufanya tufuatilie kwa karibu yanayotokea ndani ya chama hicho.

Nimeisikiliza na nimeisoma hotuba ya Kikwete. Tafsiri yangu;
Kikwete anasema; ” Chama cha Mapinduzi kiige tabia ya nyoka ya kila baada ya muda fulani hujivua gamba lake na kupata jipya. Hatuna budi kufanya hivyo na kufanya hivyo sasa” . Anasema Kikwete.

Naam. CCM ya Jakaya Kikwete ni nyoka anayejibua. Kwa nyoka kujibua kuna maana ya mabadiliko. Nyoka kutoa gamba lake ni mabadiliko makubwa katika mwili wake.

Kwa kumsikiliza na kumwangalia Kikwete sina hofu juu ya dhamira yake ya moyoni . Kikwete anaonyesha kukiona kile ambacho wengi ndani ya chama chake, ama wamekiona lakini hawataki kukiona au hawajakiona. Kikwete ameshauona upepo wa mabadiliko unavyovuma.


Kuna wimbi la mabadiliko linaendelea barani Afrika. Vijana ndio wenye kuongoza harakati hizo za mabadiliko. Watanzania hatuna sababu ya kupoteza muda kujadili na kujiuliza kama tunahitaji mabadiliko au la? Ukweli ni huu, wimbi la MABADILIKO linakuja. Tunachokiona sasa ni upepo unaovuma kabla wimbi lenyewe kutua.


Siamini kama ya Tunisia na Misri yanaweza kutokea Tanzania. Kuna tofauti kubwa. WaTunisia Na WaMisri wamechoshwa na Usultani. Mtu mmoja na familia yake kuongoza maisha. Wakati Hosni Mubarak ametawala kwa miaka 30, ndani ya miaka 30 hiyo Watanzania tumekuwa na marais watatu. Yetu ni matatizo mengine. Tunafanya uchaguzi kila baada ya miaka mitano. Tunachohitaji ni Marekebisho makubwa ya Katiba yetu ili , mbali ya kuboresha mambo mengine, tuwe na chaguzi huru na za haki.


Ni jambo jema kwa CCM na Watanzania kwa sasa, kuwa Mwenyekiti wa CCM na Rais wa nchi haitwi Benjamin Mkapa. Kikwete ni plagmatic , si dogmatic na teknokrati kama mwenzake aliyemtangulia. CCM inamhitaji kiongozi wa mfano wa Kikwete kulikabili wimbi la mabadiliko linalokuja.


Nilishapata kuandika miaka minne iliyopita, kuwa Jakaya Kikwete, kama Rais na
Mwenyekiti wa chama tawala, hana jinsi, bali ana lazima ya kufanya mabadiliko makubwa katika
safu za uongozi ndani ya chama chake na serikalini. Jambo hilo lilipatwa kufanywa na
Mwalimu Nyerere miaka kumi baada ya Azimio la Arusha.

Ikumbukwe, juma moja baada ya kuzaliwa kwa CCM tarehe 5 ya mwezi wa pili,
mwaka 1977, Mwalimu Nyerere alifanya mabadiliko makubwa ya uongozi wa Chama
na Serikali. Yale ya mwaka 1977 yanabaki kuwa ni mabadiliko makubwa ya kihistoria
kuwahi kufanywa na kiongozi wa Tanzania tangu tupate uhuru.

Yalikuwa ni mabadiliko makubwa ya Baraza la Mawaziri yaliyogusa karibu wizara zote. Ni
mabadiliko yale yaliyopelekea Bw. Pius Msekwa kufanywa kuwa Katibu Mkuu Mtendaji
wa Kwanza wa CCM.


Kikwete na CCM wana mtihani mkubwa kama wanataka kubaki katika uongozi ifikapo mwaka 2015. Swali moja gumu wanalotakiwa kulijibu ni hili: Ni kwa namna gani watalifikia kundi kubwa la vijana ambao sio tu wanaonyesha kuchoshwa na chama hicho, bali wanawaona hata baadhi ya viongozi ndani ya CCM kuwa ni watu wasiokwenda na wakati.
Dunia Imebadilika. Nahitimisha.
Maggid
Iringa
Februari 6, 2011


MFUMO WA BODI YA MIKOPO TZ


RAIS Jakaya Kikwete ameteua tume ya wataalamu 11 kufanya mapitio ya mfumo wa uendeshaji wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kwa lengo la kuboresha utoaji wa mikopo.

Katika hadidu za rejea, tume hiyo imeagizwa kuangalia upya vigezo na sifa zinazozingatiwa katika utoaji wa mkopo endapo vinakidhi haja na mahitaji halisi ya waombaji na taifa kulingana na makusudio ya kuundwa kwa bodi hiyo.

Kabla ya kuangalia vigezo hivyo, tume hiyo imeagizwa kuchambua kwa kina Sheria iliyounda bodi hiyo na kanuni zake na kubainisha vifungu vinavyohitaji marekebisho kulingana na hali halisi ya utoaji mkopo.

Akizungumza mkoani hapa jana, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema tume hiyo imetakiwa kufanya kazi kwa muda wa siku 60 kuanzia Februari 14 mwaka huu na kuwasilisha ripoti yake kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo Aprili 15, mwaka huu.

Alisema pia imeagizwa kuangalia kwa kina muundo wa bodi na ufanisi wake katika utoaji na urejeshwaji wa mikopo na kutoa mapendekezo.

Mbali na muundo pia imetakiwa kuchunguza kiini cha malalamiko na uhusiano usioridhisha kati ya bodi na wanafunzi, bodi na taasisi ya elimu ya juu na kati ya bodi na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na katika mapendekezo, yawepo ya namna ya kurejesha uhusiano mzuri.

Katika kufanya kazi yao wajumbe wa bodi hiyo wameagizwa kuangalia nchi nyingine zenye mazingira kama ya Tanzania zilizofanikiwa kugharimia elimu ya juu kwa mfumo wa mikopo. Lengo lake ni kuwezesha mikopo itolewe kwa wanafunzi wengi wahitaji wa elimu ya juu bila lawama na kuboresha mfumo huo kwa kadiri inavyoonekana inafaa.

Hatua hiyo ya Serikali, imechukuliwa kukiwa na shinikizo kutoka kwa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), wa kuipindua au kuivunja bodi hiyo na kuundwa upya.

Shinikizo hilo la UVCCM, lililotolewa na Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la umoja huo wakidai ndio suluhisho la migomo iliyokuwa ikilipuka kutoka katika vyuo vikuu zaidi ya 10 sasa huku kero kuu ikiwa kucheleweshewa mikopo.

Hata hivyo, uundwaji wa tume hiyo, ambao uliahidiwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa mara tu alipofanya ziara ya kwanza kutembelea bodi hiyo, umeonekana kutofuata shinikizo hilo la UVCCM.

Mbali na ahadi hiyo, hata tamko la bodi hiyo lililotolewa siku chache baada ya tamko la UVCCM kutaka ipinduliwe, lilieleza kuwa changamoto iko katika mfumo na kwamba hata ikivunjwa, watakaorithi mfumo huo watakumbana na changamoto hiyo hiyo.

Katika tamko hilo la HELSB, ambalo lilitamka wazi kwamba UVCCM walikurupuka, bodi hiyo ililaumu Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) na menejimenti za vyuo husika kwa kuchelewesha majina ya wanafunzi wanaopaswa kupewa mikopo.

Hata hivyo, UVCCM katika moja ya malalamiko yaliyokuwepo katika shinikizo hilo, lilikuwepo la mtindo wa bodi hiyo kupeleka fedha za wanafunzi hao kwa uongozi wa vyuo badala ya akaunti binafsi za wanafunzi.

Malalamiko hayo ya kutupiana lawama yameonekana kuzingatiwa, kwani wataalamu wa tume hiyo ya Rais, wamechaguliwa kwa uwakilishi kuunda sura ya Muungano na kutoka menejimenti za vyuo vikuu vya umma na binafsi na TCU zilizolalamikiwa na bodi.

Pia wapo wawakili wa serikali za wanafunzi, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, wahadhiri na wataalamu wa benki na kutoka kwa wadau wengine wa elimu zikiwemo asasi za jamii.

Kati ya wajumbe hao yupo Mwenyekiti ambaye ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anayehusika na Taaluma, Profesa Makenya Maboko na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro, Kassim Almas Umba anayehusika na Utawala wa Fedha.

Pia yupo Ofisa Uhusiano wa Kimataifa wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Zanzibar, Masoud Mohamed Haji na Mhadhiri Mwandamizi wa elimu kutoka Chuo Kikuu cha Tumaini Arusha, Dk. Eliawony Meena.

Wengine ni Naibu Katibu Mkuu TCU, Daniel Magwiza, Mkurugenzi Msaidizi (Uandishi Sheria) kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Sarah Baharamoka na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi Inayopigania Elimu kwa Wanawake tawi la Tanzania, Profesa Penina Mlama.

Wengine ni Ofisa Taaluma Chuo cha Usimamizi wa Fedha, Deo Daudi ambaye alikuwa Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso) kwa mwaka 2006/2007.

Rais pia amemteua katika bodi hiyo Mkurugenzi wa Mikopo Benki ya CRDB, Anderson Mlambwa, Mkurugenzi wa Elimu ya Juu, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Wilbert Abel na Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Elimu Tanzania, Rosemary Rulabuka.

CHANZO: HABARILEO

Saturday, February 5, 2011

SANGOMA MTOA MAPEPO MORO


Pembe kubwa linalodaiwa kutolewa nje ya nyumba ya mkazi mmoja wa Mtaa wa Mtoni mjini Morogoro na Sangoma huyo.
MGANGA wa jadi (sangoma) anayefahamika kwa jina moja la Dk. Muzinga, jana jioni alitoa pembe kubwa nje ya nyumba ya mkazi mmoja wa Mtaa wa Mtoni mjini Morogoro, Bw. Said Ally (mwenye T-shirt ya Salama).

Akizungumza na matandao huu, sangoma huyo kijana alidai kwamba alipokea maombi kutoka kwa Bw. Ally akitaka nyumba yake ifanyiwe uchunguzi.

"Baada ya mteja wangu kuhisi mambo tofauti kwenye nyumba yake, alikfika hapa ofisini kuomba huduma yangu. Nilifika kwake na kioo changu kikanionyesha kwenye shimo lililo nyuma ya nyumba yake kwamba kuna pembe.

Nilipofukua nimelikuta hili pembe na nikaamua kuliteketeza na moto, " akasema Sangoma huyo.

Tukio hilo linaonyeshwa katika picha zifuatazo:


Friday, February 4, 2011

ALLY CHOKI AMCHOKONOA ASHA BARAKA

Wanamuziki wapya wa Extra Bongo wakiwa katika picha ya pamoja kabla ya utambulisho.

BENDI ya muziki wa dansi nchini, African Stars International (Twanga Pepeta) leo imepata pigo jingine tena baada ya kuondokewa na wanamuziki wake wengine watano kujiunga na bendi ya Extra Bongo inayomilikiwa na Ally Choki Rwambo (Mzee wa Farasi).
Utambulisho wa wanamuziki hao wapya kwa waandishi wa habari umefanyika leo katika ukumbi wa Meeda uliopo Sinza Mori jijini Dar.
Akizungumza kabla ya kuwatambulisha wanamuziki hao, Choki amesema sasa ni zamu ya bendi yake kulikamata jiji, hivyo aliwaomba mashabiki wake wakae tayari kuipokea Extra Bongo mpya.
Wanamuziki hao ni: Issack Buriani ‘Super Danger’, Saulo John ‘Ferguson’, Rogert Hegga ‘Caterpilar’, Otilia Boniface ‘Kandoro’ na Hassan Musa ‘Nyamwela’.
Wanamuziki wengine kutoka nje ya Twanga Pepeta ni Oseah pamoja na George Kanuti waliokuwa wakifanya shughuli za muziki nchini Muscat.



Mkurugenzi wa Extra Bongo, Ally Choki, aliyenyoosha mkono akimtambulisha mpiga gitaa la besi (Oseah) aliyevaa kofia na miwani.


‘Ferguson’ akitafakari jambo.

Ally Choki akimtambulisha Otilia Boniface ‘Kandoro’.

Mzee wa Kisigino (Ferguson) akiwa katika pozi.

MANJI AMPONDA MENGI


Mkurugenzi wa Kampuni ya Quality Group, Yusuph Manji (kulia) akiongozana na Katibu wake, Mhingo Rweyemamu, wakati wakiingia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam Jana mchana kwa ajili ya kuwasilisha vielelezo na kutoa ushahidi katika kesi yake dhidi ya Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Regnald Mengi. Katika kesi hiyo Manji alimtaka Mengi kumlipa fidia ya Sh 1 tu pamoja na kumuomba radhi kupitia Televisheni yake ya ITV kwa muda wa siku saba mfululizo.


Yusuph Manji, akizungumza na wakili wake Mabele Marando, wakati alipoingia kwenye Chumba cha mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam jana, kwa ajili ya kutoa ushahidi na kuwasilisha vielelezo vya kesi yake dhidi ya Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP, Regnald Mengi.


Manji akipitia faili lake kabla ya kuingia katika chumba cha Mahakama kuanza kutoa ushahidi.

MFANYABIASHARA maarufu jijini Dar es Salaam, Yusuf Manji, ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, kuwa tuhuma zote dhidi yake zilizotolewa na Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP Ltd, Reginald Mengi, za kuwa ni fisadi papa, ni uzushi mtupu na zimemshushia hadhi yake.

Akitoa ushahidi leo mbele ya Mahakama hiyo, Manji alisema kutokana na kauli aliyoitoa Mengi kupitia vyombo vya habari, imesababisha aonekane mtu asiyefaa katika jamii, na familia yake inataka kumtenga.

“Tuhuma zilizowekwa na Mengi zimeshusha heshima yangu katika jamii, wafanyakazi wangu, familia za wafanyakazi wangu, wabunge hata familia yangu na familia inataka kuondoka,” amedai Manji.

Manji ametoa madai hayo katika kesi hiyo ambayo anadai fidia ya Sh moja kwa madai ya kudhalilishwa na Mengi katika kipindi kilichorushwa kupitia vituo vyake vya televisheni na kwenye magazeti.

Akielezea hadhi aliyonayo mbele ya jamii, Manji alidai kuwa klabu ya soka ya Yanga imemteua kuwa mfadhili, na pia alionesha baadhi ya barua ambazo zilikuwa zikimpa mialiko katika shughuli mbalimbali za kijamii ikiwamo ya mahafali ya kumaliza kidato cha sita kwa wanafunzi wa Shule ya Benjamin Mkapa, jijini.

Kesi hiyo iko mbele ya Hakimu Aloyce Katemana, na Manji anawakilishwa na mawakili Mabere Marando, Beatus Malima, Dk. Ringo Tenga na Richard Rweyongeza.

Manji aliwasilisha mahakamani CD ya video iliyokuwa ikionesha Mengi akiongea kupitia televisheni na akimtaja Manji kuwa ni fisadi papa na kwamba anawanyonya watu wa hali ya chini.

Manji alidai tuhuma hizo si za kweli, bali anajishughulisha na kuwasaidia watu.

Aidha, alikanusha kumiliki nyumba Amerika na Afrika Kusini, akidai hana nyumba yoyote aliyoinunua yeye, bali nyumba zote ni za baba yake ambaye alifariki na kumuachia mama yake ambaye kuna nyumba ambazo alimpatia kama zawadi, na kwamba hata nyumba anayoishi ni ya baba yake.

Alidai Mengi pia amemtuhumu kumtishia maisha yake kuwa atamuua jambo ambalo hajawahi kulifanya, “Hii sio mara ya kwanza Mengi kunituhumu kumtishia maisha yake mara kadhaa amefanya hivyo,” amedai Manji.

Wakati huo huo, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemtaka Mhasibu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Lilian Chengula anayetuhumiwa kuiba fedha za shirika hilo Sh bilioni 1.3, kuwasilisha ombi la dhamana Mahakama Kuu kwa sababu Mahakama hiyo haina kibali cha kusikiliza shauri la uhujumu uchumi.

CHANZO: HABARILEO