Social Icons

Friday, February 4, 2011

NOTI MPYA ZAITIKISA BOT

Gavana Mkuu wa Benki Kuu ya Tanzania Prof.Benno Ndulu akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam Kuhusu noti mpya zinazotumika nchini kuwa zina ubora na viwango vya kimataifa na kuwataka wananchi kuwa makini katika kufuatilia na kuzitambua alama muhimu za noti halali ikiwemo ile ya kutoa rangi pindi inaposuguliwa kwenye karatasi nyeupe. Kulia ni Mkurugenzi wa Huduma za Kibenki (BOT) Bw. Emmanuel Boaz.
*MTAALAMU KUTOKA NJE ALETWA KUTHIBITISHA UBORA
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imelazimika kumleta nchini, Mkurugenzi wa Kampuni ya Crane Curreny, ya Sweden iliyoshinda zabuni ya kutengeza noti mpya zilizoanza kutumika Januari mwaka huu, kueleza ubora wake baada ya noti hizo kuhisiwa kuwa zinachuja na ni rahisi kughushiwa.

Ujio wa mtaalamu huyo, Peter Brown ni utekelezaji wa ahadi ya Gavana wa BoT, Professa Benno Ndullu aliyoitoa wiki mbili zilizopita kuhusu taasisi yake kufuatilia ubora wa noti mpya ambao ulianza kutiliwa mashaka na baadhi ya wananchi.

Januari 23, mwaka huu gazeti hili liliripoti habari ya uchunguzi iliyoelezea mashaka kuhusu ubora wa noti hizo mpya, baada ya kubainika kuwa baadhi zinachuja na kuacha rangi zikilowa maji au jasho.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo, noti hizo hasa za Sh5,000 na Sh10,000 pia zilibainika kuwa zikikandamizwa kwenye karatasi nyeupe bila kulowanishwa na maji au jasho, huacha rangi.

Hali hiyo ilisababisha baadhi ya watu kuanza kutilia mashaka ubora wake, huku wasomi wakitaka Serikali kuwa makini kwa kuwa inaweza kupata hasara kubwa.

Katika kufuatilia suala hilo, Gavana Ndulu aliliambia Mwananchi kwamba BoT itafuatilia utta huo ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na mzabuni ambaye ni kampuni ya Crane Currency ili kasoro zinazojitokeza ziweze kurekebishwa mara moja.

Maelezo ya mtaalamu Brown

Jana, Brown ambaye ni Mkurugenzi Mauzo wa Kampuni ya Crane Currency, Kanda ya Afrika alitoa ufafanuzi kuhusu ubora wa noti mpya ili kuondoa mashaka yaliyojitokeza.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Brown alisema kutoa rangi ni moja ya alama za usalama na ubora wa noti hizo.

Brown alifafanua kuwa noti hizo zimetengenezwa kwa teknolojia ijulikanayo kama ‘Intaglio’ ambayo imekuwa ikitumika kwa muda mrefu katika kuchapisha noti mbalimbali duniani. Alisema teknolojia hiyo inatoa uhakika mkubwa wa usalama wa noti.

Brown alifika nchini juzi na jana alifanya mkutano na uongozi wa BoT na kusema kampuni yake imekuwa ikichapisha noti mbalimbali duniani, zikiwemo dola za Marekani na kwamba noti zote zilizochapishwa kwa kutumia teknolojia hiyo huwa na wino mwingi katika kingo zake.

Kampuni hiyo ya Crane Currency yenye makao yake nchini Sweden ndio iliyoshinda zabuni ya kuchapisha noti mpya za shilingi 500, 1,000, 2,000, 5,000 na 10,000.

Akifafanua juu ya madai kuwa noti hizo zikilowa kwa jasho au maji zinatoa rangi, Prof Ndulu alisema uchujaji huo hauwezi kumaliza rangi iliyotumika katika utengenezaji na kwamba noti hizo zinaweza kuendelea kuwa katika ubora ule ule kwa muda mrefu.

“Noti zote hizi zinapotengenezwa kiwandani, zinapitishwa kwenye test (majaribio), zinawekwa kwenye maji, zinapitia cycles (mizunguko) yote na zinapotoka zinatakiwa zibaki vilevile,” alifafanua.

Maelezo ya Gavana Ndulu

Gavana Ndulu kwa uapnde alieleza kuwa noti hizo kutoa rangi wakati zimesuguliwa kwenye karatasi au kulowana ni moja ya alama zake za usalama.

Hata hivyo, wakati BoT wakitangaza katika vyombo vya habari kuhusu alama za usalama (security features) katika noti hizo, hawakuwahi kutaja hilo la kuchuja kwa rangi za noti hizo kuwa miongoni mwa vigezo vya ubora wake.

Ndulu alisema rangi hiyo inyotoka katika noti hizo, huwezi kuiona katika noti bandia na kwamba teknolojia iliyotumika inasaidia noti hizo kukaa muda mrefu bila kuchakaa.

Prof Ndulu aliwaambia waandishi wa habari kuwa hata noti za zamani za Sh 5,000 na 10,000 pia zikisuguliwa kwenye karatasi huacha rangi.

“Ukitaka kujua noti halali, kama ukiisugua kwenye karatasi, lazima iache rangi na rangi inapokuwa imekolea zaidi, inaacha zaidi,” alisema Prof Ndulu na kuongeza:

"Noti bandia haziwezi kuacha rangi kwa kuwa hazikutengenezwa kitaalamu na hiyo ni njia nzuri kwa mtumiaji kugundua noti bandia na noti halali na pia noti ikiwa na rangi nyingi inakuwa ni imara na haichakai mapema".

Kuhusu kuwepo kwa noti za zamani na za sasa katika mzunguko wa fedha alisema noti zote ni halali na zitaendelea kutumika hadi zile za zamani zitakapoisha kwenye mzunguko.

Prof Ndulu alisema noti hizo zitachukua mwaka mmoja kupotea, hivyo zote zitaendelea kuwa halali kwa manunuzi ya nchini.

Alisema hivi sasa kuna watu wameshaanza kutengeneza noti bandia na tayari ameshaiona moja ya aina hiyo na kufahamisha kuwa suala la kubadili fedha kila baada ya muda linatokana na kuwakwepa wajanja ambao hutengeneza bandia.

Akizungumzia akiba ya fedha za kigeni ambayo Tanzania inayo hadi hivi sasa, Prof Ndulu alisema kuwa nchi ina dola za Marekani 3.8 bilioni ambazo zinaweza kununua huduma kwa nchi nzima kwa miezi sita mfululizo.

Alisema kiasi hicho cha fedha ni kikubwa kupita nchi yeyote ya Afrika Mashariki.

"Hatuna shida kwenye hilo kwa kuwa hata kwa benki za biashara zina kiasi cha Sh1 bilioni na watu wa kawaida wana Sh1.5 bilioni,"alisema Prof Ndulu na kuongeza kuwa nchi kwa ujumla ina zaidi ya Sh5 bilioni ya fedha za kigeni.

Mtazamo wa Jamii
Baadhi ya watu waliowasiliana na gazeti hili wamelalamikia tatizo la noti mpya kuchuja na kuitaka Benki Kuu (BoT) kulifuatilia kwa karibu na kulipatia ufumbuzi.

Lawrence Mkina ambaye mkazi wa jijini Dar es Salaam aliiambia Mwananchi kwa njia ya simu kuwa haamini kama noti mpya zina ubora unaotakiwa.

Alisema aliweka noti mpya za Sh 5,000 lakini kwenye mfuko wa shati jeupe baadaye alipozitoa shati lilikuwa limechafuka kwa rangi ya noti hizo.

Mkina alidai kuwa huenda noti hizo zitakuwa ‘zimechachakuliwa’ na wanjanja mitaani kwani hata ukiisugua katika karatasi nyeupe inaacha rangi kama vile carbon paper.

Ili kuthibitisha madai hayo, gazeti hili ilichukua noti mpya ya Sh 5,000 na kuisugua kwenye karatasi ya nyeupe na noti hiyo iliacha rangi nyingi ya bluu.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Honest Ngowi alieleza madhara ya noti zisizokuwa na ubora kuwa ni pamoja na kugushiwa kirahisi.

“Ubora wa noti ni kitu muhimu na kama ikikosa ubora inaleta maswali mengi na moja ya athari itakayojitokeza ni kugushiwa kirahisi,’’ alisema Dk Ngowi.

Dk Ngowi ambaye ni mwanazuoni aliyebobea katika taaluma ya uchumi, alisema noti ikikosa ubora, huchakaa mapema na kuleta utata katika kukubalika kwenye soko.

“Kutokana na kuchakaa mapema, serikali italazimika kuchapisha noti nyingini hali ambayo italigharimu taifa fedha nyingi katika muda mfupi. Pia inawezekana nchi za Jumuiya ya Afrika ya Afrika Mashariki, zikakataa kuzitumia noti hizo,’’ alisema.

Kuhusu sifa na ubora wa noti, Dk Ngowi alisema ni lazima iwe katika kiwango bora ikiwamo kuwa na karatasi ngumu isiyochakaa na kuchanika mapema na kuwa na uzito.

“Noti yenye ubora ni lazima iwe na sifa ya Durabillity, isiyoharibika mapema na iwe nzito,’’ alisema Dk Ngowi.

Ahadi ya Gavana

Kutokana na hali hiyo, Gavana Ndullu, alisema BoT inafuatilia kwa karibu matatizo yanayojitokeza katika noti hizo mpya na kuyafanyia kazi.

“Hili linawezekana ingawa wewe ndio mtu wa kwanza kujitokeza kueleza, lakini kama tatizo hili lipo, tutalifanyia kazi,’’ alisema Profesa Ndullu.

Akaongeza: “ Kwa sasa BoT ina monitor (Fuatailia) kwa ukaribu usambazaji wa noti mpya pamoja na kuangalia matatizo yanayojitokeza na kuyafanyia kazi haraka iwezekanavyo.’’

Gavana huyo alisema matatizo yote yatakayojitokeza katika noti hizo yatafikishwa kwa mzabuni aliyezichapisha ili kufanyiwa kazi.


CHANZO: MWANANCHI

FFU WAVAMIA OFISI ZA GLOBAL PUBLISHERS LEO

Askari wa kutuliza ghasia (FFU) wakijaribu kumchukua mmoja wa wafanyakazi wa Global Publishers, Hassan Ally Daffa kwa madai kuwa ni mmoja wa wanafunzi walioandamana huku wafanyakazi wenzake wakimtetea.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Askari wa kutuliza ghasia (FFU) leo asubuhi badala ya kutuliza walikuwa chanzo cha fujo pale walipoingia kama wendawazimu katika ofisi za Kampuni ya Global Publishers na kuanza kupiga makofi na mabomu wafanyakazi.

Polisi hao walifika katika ofisi hizo ghafla huku wakiwa na bunduki na kuanza kufyatua mabomu ya machozi na baadaye polisi kadhaa waliingia ndani huku wakiwa wameshikilia bastola maalum ambapo kulikuwa na kikao cha kupitia magazeti kikiendelea, polisi mmoja alitoka nje na mtumishi mmoja. Kifupi hali ilikuwa mbaya kutokana na kipigo cha polisi hao kwa wafanyakazi wasiokuwa na hatia.

Kuona hali inazidi kuwa mbaya, Mhariri Mtendaji Manyota aliwasiliana na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, (IGP) Saidi Mwema na kumueleza kila kitu kuhusiana na fujo za kikosi cha kutuliza ghasia ambapo kiongozi huyo alishtuka na kutoa pole huku akiahidi kushughulikia suala hilo.




WANAFUNZI WA CHUO CHA USAFIRISHAJI DAR WAMZUIA MKUU WILAYA YA KINONDONI KUINGIA CHUONI .

Baadhi ya wanafunzi wa chuo hicho wakiwa wametanda getini kuwazuia polisi kuingia chuoni hapo.

WANAFUNZI wa chuo cha usafirishaji (NIT) kilichopo Mabibo jijini Dar jana walimzuia mkuu wa wilaya ya Kinondoni Jordan Rugimbana kuingia chuoni wakisema wamechoshwa na dharau za wakuu wao wa chuo na walimtaka mkuu huyo wa wilaya kwenda chuoni hapo na waziri husika ili kujadili matatizo yao.

Hata hivyo, baada ya majadiliano, Rugimbana aliruhusiwa kuingia chuoni hapo ambapo wanafunzi, wakiongozwa na rais wa serikali yao, Seif Khamis, walielezea matatizo yao wakitaka yatatuliwe mara moja .



Magari ya viongozi wa Wilaya ya Kinondoni yakiwa nje baada ya kuzuiwa kuingia chuoni.

Rais wa chuo hicho, Seif Khamisi (kulia), akiainisha mbele ya mkuu wa Wilaya Jordan Rugimbana (wa tatu kulia) na viongozi wa serikali kilichowafanya wagome.

Moja ya mabango yaliyokuwa getini likiwa na ujumbe wa kumkataa kaimu mkuu wa chuo hicho.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Jordan Rugimbana, akiongea na wanafunzi muda mfupi baada ya kuruhusiwa kuingia katika ukumbi wa chuo hicho.

Thursday, February 3, 2011

MGAMBO KAZINI

KAMERA yetu mchana huu imewanasa mgambo wa Manispaa ya Morogoro wakiwa na bidhaa walizowapora wafanyabiashara ndogondogo waliokiuka agizo la kutofanya biashara kando ya barabara za mji huo.
Picha zifuatazo hapa chini ni baadhi ya akina mama waliokuwa wanakimbia kunusuru bidhaa zao zisichukuliwe na Mgambo hao:



NSSF WAJITOA KUZALISHA UMEME


Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umesema umeanza mchakato wa kuzalisha megwati 300 za umeme na kuziingiza katika grid ya taifa ifikapo Desemba mwaka huu, ili kusaidia kuondoa matatizo ya umeme yanayoikumba nchi kwa sasa.Mpango huo ulitangazwa jana na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk. Ramadhan Dau, jijini Arusha.
Dk. Dau bila kutoa ufafanuzi kuhusu mahali ambapo umeme huo utazalishwa, alisema tayari mfuko wake umeshateua mtaalamu mshauri kwa ajili ya kutekelezwa kwa mradi huo, ambao pia hakutaja gharama zake.

Hatua hiyo imekuja wakati nchi ikikabiliwa na matatizo ya umeme na kulilazimisha Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco) kutangaza mgawo mara kwa mara.
Dk. Dau alikuwa akizungumza katika mkutano wa wadau wa NSSF unaofanyika jijini hapa na kuhudhuriwa pia na wawakilishi wa mifuko ya hifadhi ya jamii kutoka nchi jirani za Kenya, Uganda na Burundi.
Aidha, Dk. Dau alisema kuwa mfuko wake unaangalia uwezekano wa kutandaza bomba la gesi kutoka Mnazi Bay hadi Dar es Salaam na Mwanza.
“Madhumuni ni kusambaza gesi inayozalishwa hapa nchini katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu,” alisema Dk. Dau bila kutoa ufafanuzi zaidi kuhusiana na mradi huo.
Kuhusu wanachama wa mfuko huo, Dk. Dau alisema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, wameongezeka kutoka 380,000 mwaka 2005/06 hadi 506,216 mwaka 2009/10 ambalo ni sawa na ongezeko la asilimia 33.
Alisema ifikapo Juni mwaka huu wanachama wanategemewa kufikia 518,410.
Kwa upande wa makusanyo, alisema yameongezeka kutoka Sh. bilioni 126.96 hadi Sh. bilioni 315.31 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 148.
“Mategemeo yetu ni kukusanya kiasi cha Sh. bilioni 404.58 ifikapo Juni mwaka huu,” alisema.
Akizungumzia uwekezaji, Dk. Dau alisema shirika limeendelea kuwekeza raslimali katika miradi ya muda mfupi na mrefu. Kutoka mwaka 2005/6 hadi 2009/10 uwekezaji wa Mfuko uliongezeka kutoka Sh. 424.89 bilioni hadi Sh. trilioni 1.03.
Alisema uwekezaji huu umesaidia kuongeza ajira na kuboresha thamani ya shirika.
Kuhusu ulipaji wa mafao, alsema Oktoba mwaka jana, NSSF ilipandisha pensheni kwa asilimia 52 ambapo kutokana na mabadiliko hayo kiwango cha chini cha pensheni kwa wastaafu kimeongezeka kutoka Sh. 52,000 hadi Sh. 80,000 kwa mwezi.
Katika hatua nyingine, Dk. Dau alisema tathmini inayoishia Juni 2009, imeonyesha kuwa NSSF inaweza kujiendesha, hata kama shirika litaacha kukusanya michango na bila kupata mapato yo yote kutoka katika vitega uchumi vyake, bado linaweza kuendelea kutoa mafao yote saba na kukidhi gharama za uendeshaji kwa muda wa miaka saba.
Akifungua mkutano huo kwa niaba ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka, aliipongeza NSSF kwa kujizatiti kuanza ujenzi wa daraja la Kigamboni na mipango ya kuzalisha megawati 300 za umeme na kuziweka katika gridi ya taifa pamoja na kusafirisha gesi asilia.
“Hii ni mipango mizuri na ni endelevu kwa ustawi na maendeleo ya taifa. Ujenzi wa daraja la Kigamboni ambao kwa muda mrefu wananchi walitarajia kuwa litajengwa sasa watapata faraja kusikia kuwa utaanza wakati wowote,” alisema.
“Kuhusu ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme ni jambo la muhimu zaidi na ni muafaka kwa uchumi wa taifa kwani upungufu wa umeme/kukatika mara kwa mara kwa umeme kunaathiri sana mitambo ya uzalishaji wa bidhaa viwandani, tija na ufanisi katika maofisi kupungua na hivyo kuleta athari kwa taifa,” alisema.
“Lakini athari kubwa zaidi ni ile ya kukimbiza vitega uchumi kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza wa ndani na nje ya nchi na hivyo kusababisha ajira kwa wananchi kukosekana,” alisema, na kuongeza:
“Jitihada hizi zinazofanyika na NSSF zitapunguza sana kama si kuondoa kabisa kero hizi.”
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa NSSF, Abubakar Rajabu, aliiomba serikali kutoa uamuzi wa kuukubalia mfuko huo kujenga majengo ya ofisi za ubalozi wa Tanzania nje ya nchi ili kuokoa fedha za serikali kwa kupanga ofisi.


CHANZO: NIPASHE

Wednesday, February 2, 2011

BONANZA LA TIMU YA MAUZO YA TIGO JIJINI DAR


Mkuu wa Mauzo wa Tigo Tanzania, Brahim Nallar (kushoto) akikabidhi zawadi ya friji kwa Elirehema Nyiti aliyeibuka mshindi wa jumla wa kitengo cha kuuza laini za kampuni hiyo katika bonanza la timu ya mauzo ya Tigo jijini Dar es Salaam jana. Katikati ni Mkuu wa Msoko, Gabriel Cosp.

Meneja Mauzo wa Tigo Dar es Salaam, Raymond Nkya (katikati) akikabidhi zawadi ya television kwa Vicent Paul aliyeibuka mshindi kitengo cha Tigo Rusha hiyo katika bonanza la timu ya mauzo ya Tigo jijini Dar es Salaam jana. Kushoto ni Mkuu wa Mauzo wa Tigo Tanzania, Brahim Nallar.

Mchezaji wa timu ya mauzo ya Tigo, Mariam Mussa (kulia) akiutawala mpira katika mchezo wa netiboli kati ya timu za Tigo na Habours Club wakati wa bonanza la timu ya Mauzo ya kampuni hiyo jijini Dar es Salaam jana. Katikati ni Fadhila Saidi na Mwajuma Ali wote wa Tigo. Tigo ilishinda kwa 25-23.

Mchezaji wa timu ya mauzo ya Shekilango Abdallah Sudi (kulia) akichuana na Isaya Mwaikenda wa Kariakoo katika mchezo wa soka wakati wa bonanza la timu ya mauzo ya Tigo jijini Dar es Salaam jana. Shekilango ilishinda kwa magoli 2-0.

Wachezaji wa timu ya mauzo Tigo wakishangilia mara baada ya kuwachapa Habours kwa magoli 25-23 katika mchezo wa netiboli wakati wa bonanza la timu ya mauzo ya Tigo jijini Dar es Salaam jana.

JK KUZINDUA SHIRIKISHO LA WASANII NCHINI

Rais wa Shirikisho hilo, Simon Mwakifamba, akizungumza na wanahabari katika ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Jijini Dar, juu ya tamasha hilo leo asubuhi.

RAIS Jakaya Kikwete, anatarajiwa kuzindua shirikisho la filamu hapa nchini, katika tamasha la The Mwalimu Nyerere Film Festival linalotarajiwa kufanyika Februari 14 mpaka 19 mwaka huu katika viwanja vya Leaders Club jijini Dar es Salaam.


Sehemu ya wanahabari wakifuatilia mkutano huo.

Michael Sangu a.k.a Mike (kulia) akimueleza jambo, Rais wa zamani wa wasanii, Mashaka Matongo a.k.a Abiola (mwenye tai) baada ya mkutano huo.