Social Icons

Friday, January 28, 2011

MIYEYUSHO NA FUNDI KUKAMUANA KESHO


Bondia Juma Fundi (kushoto) akipimwa afya kabla mpambano.
MABONDIA Francis Miyeyusho na Juma Fundi, kesho wanatarajia kupambana katika mchezo wa raundi 10 utakaofanyika katika Ukumbi wa Amana Vijana Social Jijini Dar es Salaam. Leo mchana paparazi wetu aliwanasa mabondia hao ukumbini hapo wakiwa kwenye hatua za mwisho za mpambano huo ikiwemo kupima afya zao.



Francis Miyeyusho (kushoto) na Fundi wakitunishiana misuli.

Promota wa pambano hilo, Kaike Siraj (katikati) akiwainua mikono juu mabondia hao kuwatakia mchezo mwema.

Aliyewahi kuwa mshindi wa Shindano la Bongo Star Search (BSS),Jumanne Idd naye alinaswa eneo la tukio na kudai atawatumbuiza mashabiki kabla ya mpambano huo.

HAYA NDO' MALEZI BORA YA BABA NA MAMA

USTADHI mmoja (pichani) jana mchana analinaswa na kamera yetu mjini Morogoro akiwa amembeba mtoto wake mgongoni na upande wa kitenge akiwa anaendesha baiskeli kuelekea sehemu ambayo haikufahamika.

Hii inaonyesha jinsi jukumu la kutunza mtoto linavyotakiwa kuwa la wazazi wote – baba na mama.



POLISI WAPUNGUZIWA MSOSI

Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, (IGP) Said Mwema.

SERIKALI imeondoa posho ya upepelezi na nyumba kwa askari polisi bila maelezo katika mishahara ya miezi ya Desemba 2010 na Januari mwaka huu, Mwananchi limebaini.

Habari zilizolifikia gazeti hili jana zimeeleza kuwa, posho hizo zitaendelea kukatwa kwani baadhi ya askari waliokwishapata mshahara wa Januari, wamesema fedha hizo hazipo.

Baadhi ya askari polisi walilithibitishia Mwananchi kuhusu kukatwa kwa mishahara yao, huku taasisi husika za serikali ambazo ni polisi makao makuu na hazina, wakirushiana mpira kuhusu suala hilo.

"Ni kweli tumekatwa posho zetu zote na tatizo hilo limeanza mwezi huu," askari mmoja wa mkoani Ruvuma alilieleza gazeti hili.

Askari mwingine aliyefika kwenye ofisi za gazeti hili jana alisema anasikitishwa na hatua hiyo kwani imeharibu bajeti yote aliyoiweka kwa mwezi Januari.

"Haya mambo ya ajabu sana, watu wamekatwa posho tena bila maelezo, wanataka askari sasa waanze kuwabambikia raia kesi ili kujiongezea kipato?"alisema.

Polisi huyo alidai kuwa katika mshahara wake wa mwezi Desemba mwaka jana, alikatwa Sh150,000 jambo ambalo limemfanya akope kwa ajili ya kuwapeleka watoto shule.

"Kukatwa posho bila maelezo ni ngumu sana na kimsingi hii inatupa shida kubwa kuzoea mazingira mapya, inaonekana hawa watu wanakata pesa zetu ili wawalipe Dowans (kampuni ya kuzalisha umeme wa dharura iliyozua zogo kutokana na mkataba tata),"alisema.

Hata hivyo kukatwa kwa fedha hiyo kumeibua utata hasa baada ya uongozi wa jeshi la polisi kutupiana mpira na Wizara ya Fedha walipotakiwa kutoa maelezo kuhusu suala hilo.

Wakati polisi ikisema yenyewe haihusiki na malipo ya askari wake, Wizara ya fedha na uchimi ilisesema inaandaa malipo ya wafanyakazi kulingana na maelekezo ya mwajiri husika.

Msemaji wa polisi, Advera Senso aliliambia gazeti hili jana kuwa hawezi kuzungumzia suala hilo kwani malipo ya polisi yanafanywa na Wizara ya Fedha (Hazina).

“Hilo suala ungewauliza watu wa Wizara ya Fedha kwa sababu sisi sio watu tunaotoa mishahara,”alisema Senso na kuongeza kuwa wao huandaa malipo kisha kuyapeleka hazina kwa ajili ya malipo.

Naye Msemaji Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Ingiahedi Mduma, alisema kuwa wizara haihusiki na suala la kupanga mishahara ya watu.

"Tunacholipa wafanyakazi ni maagizo yanayotoka kwa mwajiri," alisema Mduma.

Kwa mujibu wa Mduma jeshi la polisi haliko chini ya Wizara ya Fedha bali Ofisi ya Rais - Manejimenti ya Utumishi wa Umma, kwa hiyo mishahara inayopangwa kutoka Utumishi, ndiyo inayolipwa na Hazina.

“Sisi ni kama mawakala tu suala la kulipa mishahara linatokana na mipango iliyotolewa na Utumishi na Jeshi hilo, kwa hiyo hatuwezi kubadilisha chochote tunacholetewa,”alisema.

Lakini Mduma alidokeza kuwa kuna uwezekano wa baadhi ya polisi ambao hawajalipwa fedha za pango kuwa tayari wamepewa nyumba za kuishi.

“Inategemea kama hao polisi hawajalipwa inawezekana tayari wamegawiwa nyumba kwa hiyo kile kiasi walichokuwa wanapewa kwa ajili ya makazi kimefutwa,"alisema na kuongeza:

"Au fedha za pango walizokuwa wakilipwa walikuwa wakilipwa kwa makosa. Kama ni hivyo basi, itabidi wakatwe kwa muda wote ule waliokuwa wakiingiziwa fedha hizo, hadi deni litakapomalizika.”

Alipotakiwa kuzungumzia suala hilo jana, Kamishna wa Utawala na Rasilimali wa Jeshi la polisi, Clodwig Mtweve alisema anahitaji muda kulifuatilia.

Alisema, "Ndio kwanza umeniambia, sasa ngoja niwasiliane na kitengo cha mishahara nijue tatizo ni nini." Mtweve aliahidi kuwa atatoa maelezo ya suala hilo leo.

Alipotafutwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Nahodha hakuweza kupatikana na baadaye katika mawasiliano ya simu haikupatikana, lakini msaidizi wake alisema kuwa waziri alikuwa safarini Indonesia kufuatilia shughuli za uanzishwaji mradi wa vitambulisho vya taifa.


Polisi ni miongoni mwa kada za watumishi wa umma ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikilalamikia mishahara midogo, huku malipo hayo yakielezwa kuwa kichocheo cha kukithiri kwa vitendo vya rushwa ndani ya chombo hicho cha usalama wa raia.

Ripoti ya utafiti uliofanywa na Tasisi ya Wanaharakati wa Maendeleeo barani Afrika (ForDIA) na kutolewa Januari 18, mwaka huu inaonyesha kuwa Idara ya Polisi ni kinara wa rushwa ikizitangulia idara nyingine za serikali ambazo ni Afya na Mahakama.


Kwa mujibu Fordia, polisi inaongoza kwa kupokea rushwa, huku sekta za Afya, Mahakama, Elimu, Tanesco na idara za leseni na ushuru zikitajwa pia kuwa na kiwango kikubwa cha rushwa.

Mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo Bubelwa Kaiza alisema “polisi ndio vinara wa rushwa kwa sasa”.

Alisema utafiti huo unaonyesha kuwa polisi wanaongozwa kwa asilimia 81.9 kwa kupokea na kutoa rushwa. “Polisi imeendelea kushika nafasi ya kwanza baada ya kuongoza idara nyingine kwa kuwa na asilimia 85.3 mwaka jana kutoka nafasi ya pili ya asilimia 75.8 waliyokuwa wakiishikilia mwaka 2009,’’alisema Bubelwa.

Kwa mujibu wa Fordia utafiti huo ulifanyika katika mikoa 11 ya Tanzania ambayo ni Dar es salaam, Tanga, Kagera, Manyara, Rukwa, Tabora, Kilimanjaro, Mwanza, Mara, Pwani na Mtwara.

Utafiti huo pia umejumuisha serikali za mitaa 47 katika wilaya tofauti nchini na kulishirikisha watu mbalimbali wapatao 1,122 ambao waliulizwa maswali, lengo likiwa kujua kinara wa rushwa nchini.

Kati ya watu hao 1,122 waliohojiwa wanaume walikuwa 646 na wanawake 476. Hata hivyo watu walioweza kutoa majibu walikuwa 367, ambapo wanaume walikuwa 248 na wanawake 119, huku Bubelwa akieleza kuwa watu waliohojiwa ni wanaoishi mijini na vijijini.

Alisema sula la umri lilizingatiwa katika kuwahoji watu ambapo, waliohojiwa wote walizidi miaka 18, hivyo utafiti huo kuhusisha vijana, wazee na watu wenye umri wa kawaida.

Alifafanua kuwa walipata majibu na maoni mbali mbali kutoka kwa wananchi kuhusu suala la polisi ambapo walielezwa kuwa watu hukamatwa kwa uonevu na hulazimika kutoa 'kitu kidogo' (rushwa), ili waachiwe hata kama hawakuwa na makosa, ambapo pia watu wenye makosa wanapofikishwa polisi huachiwa baada ya muda mfupi kutokana na kutoa kitu kidogo.

Alisema lengo la utafiti huo ambao ulifanyika kwa nchi nzima ilikuwa ni kuanzisha majadiliano ili kuonyesha uelewa kwa wananchi na kuipa changamoto serikali juu ya mapambano ya rushwa.

CHANZO: MWANANCHI

Wednesday, January 26, 2011

MAKAMU WA RAIS AFUNGUA SEMINA YA WABUNGE

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohamed Gharib Bilal, akipeana mikono na na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Anne Makinda katika Ukumbi wa mikutano Ubungo Plaza alikoenda kufungua Semina elekezi ya siku 10 kwa Wabunge wote wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohamed Gharib Bilal, akifunguwa Semina Elekezi ya siku 10 kwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyoanza leo katika ukumbi wa Hoteli ya Ubungo Plaza Dar es salaam.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohamed Gharib Bilal, akipunga mkono kuagana na Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kufunguwa Semina elekezi ya siku 10 kwa Wabunge hao katika ukumbi wa Hoteli ya Ubungo Plaza leo.

WANAFUNZI WA CHUO KIKUU CHA RUAHA (University College),WAGOMA

Wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa chuo cha Ruco wakiwa katika mgomo leo wakishinikiza bodi ya mikopo kuwaingiza fedha zao za kujikimu kiasi cha shilingi 300,000 kama ilivyokuwa katika vyuo vya Mkwawa cha Iringa na UDOM cha Dodoma hivi karibuni.

TWANGA, WANAUME HALISI KUKAMUA SAUTI ZA BUSARA

Msanii Juma Nature akiwa na Kiongozi wa African Stars 'Twanga Pepeta' Lwiza Mbuttu mara tu baada ya mkutano wa waandishi wa habari na waandaji wa tamasha la Sauti Za Busara jijini Dar leo. Sir Nature atakuwepo Sauti za Busara kwa mara ya pili wakati Twanga watakuwa Zenji kwa mara ya kwanza kwenye tamasha hilo. Chini ni video ya Lwiza Mbuttu akiongelea mipango ya Twanga k.

KESI YA MURO YAFIKIA PATAMU

MAHAKAMA ya Hakimu mkazi Kisutu imepokea pingu, miwani na hati ya upekuzi katika kesi ya kuomba rushwa ya sh milioni 10 inayomkabili aliyekuwa mtangazaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1) Jerry Muro kama kielelezo cha ushahidi katika kesi hiyo.Vielelezo hivyo viliwasilishwa jana mahakamani hapo na Ofisa wa Polisi dwani Nyanda ambaye ni shahidi wa sita katika kesi hiyo, mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo Gabriel Mirumbe.Shahidi huyo aliieleza Mahakama kuwa Januari 29, mwaka 2010 akiwa ofisini kwake alipokea maagizo kutoka kwa mkuu wake wa kazi Kamishina wa Upelelezi Charles Mkumbo akimtaka kufanya upekuzi katika gari yenye namba za usajili T 545 BEH mali ya Jerry Muro.Alidai alishuka kwenda kulifuata gari hilo lililokuwa limepaki kwenye maegesho ya magari ya kituo kikuu cha polisi kati akiwa na mlalamikaji Michael Wage pamoja na mashahidi wengine ili kushuhudia zoezi la upekuzi huo.“Wage aliyekuwa analalamika kutishiwa kuuawa na Muro alikuwepo makusudi ili kuitambua miwani yake aliyodai kuisahau katika gari ya Muro siku aliyokamatwa na pingu aliyodai kutishiwa kufungwa nayo.“Baada ya upekuzi huo vitu vyote vilirekodiwa na kusainiwa na mimi na Muro mwenyewe kama uthibitisho kwamba kweli vitu hivyo vilikutwa garini kwake,” alidai shahidi huyo.Katika kesi hiyo Muro na wenzake Edmund Kapama na Deogratius Mgasa wanadaiwa kuomba rushwa ya Sh milioni 10, kutoka kwa aliyekuwa Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Michael Wage, Januari 29 mwaka jana.Mwendesha mashitaka wakili Mkuu wa Serikali Boniface Stanslaus alidai kwa jana upande wa mashitaka ulikuwa na shahidi mmoja ambapo wengine watatu waliobaki watatoa ushahidi wao pindi kesi hiyo itakapopangiwa tarehe nyingine. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Machi 7 na 8, mwaka huu itakaposikilizwa tena.